baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini
Waandishi wa habari nchini wameaswa kujiepusha kuwa chanzo cha migogoro, kwa kuwa na upendeleo wakati wa kuandika ka kuripoti habari mbalimbali zinazojitokeza katika jamii.
Hayo yamebainika katika mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Njombe yaliyoanza hii leo yanayoendeshwa na baraza la habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na chama cha waandishi wa habari wa mkoa wa Njombe (NPC).
Akizungumza wakati akitoa mafunzo kwa waandishi hao mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka baraza la habari Tanzania Bw. Attilio Tagalile amesema kwa hivi sasa waandishi wengi hapa nchini wamekuwa wakibagua katika kuandika habari mbalimbali kwa kutoa kipaumbele kwa baadhi ya habari huku wakiacha kuandika na kuripoti habari nyingine zinazofanana.
"Mfano mzuri juzi tu kulikuwa na uchanguzi mdogo wa jimbo la Kalenga lakini vyombo vingi vya habari viliripoti habari za chama kimoja tu, ilikuwa rais sana kupata habari za CCM na ukitaka za Chadema labda upate gazeti la Tanzania Daima, sasa kwa nini iwe hivyo, na huo ni uandishi gani?" amesema Tagalile.
Amesema taaluma ya uandishi wa habari haitaki upendeleo wa aina yeyote kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha migogoro katika jamii ambayo kama waandishi hao wangekuwa makini isingeweza kujitokeza.
Ameongeza kuwa imezoeleka katika jamii kuwa mtu yeyote anaweza kusomea uandishi wa habari kwa kuwa ni fani rahisi jambo ambalo amedai si rahisi kama inavyoonekana kwa kuwa ni taaluma yenye maadili na nguvu hivyo kama waandishi wataendelea na upendeleo wao ni heri wakafanye kazi nyingine
"Kama unaona fani hii huiwezi ndugu yangu ni bora ukauze nyanya Ilula pale, hii fani iache huiwezi" amesema.
Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa mkoa wa Njombe kuandika habari bila upendeleo na bila kuleta madhara kwa jamii na taifa kwa ujumla