Wanahabari wakimsikiliza kwa makini
Waandishi wa habari mkoani Njombe wametakiwa kuacha kuandika habari za uchochezi kwa kuwa madhara yake ni makubwa kwao na taifa kwa ujumla
Kutokana na vyombo vya habari kuwa na nguvu, endapo vitaongoza kwa kutoa habari za uchochezi zilizoandikwa na waandishi wa vyombo hivyo ni dhahiri kuwa kutakuwa na hatari ya taifa kutumbukia katika machafuko ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na waandishi hao
Kauli hiyo imetolewa hii leo Juni 17 na mwezeshaji kutoka baraza la habari tanzania (MCT) Bw. Attilio Tagalile wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Njombe(NPC) yenye lengo la kuwajengea uwezo katika mambo mbalimbali
Amesema kwa hivi sasa kumekuwepo na kauli za kichochezi zinazotolewa na baadhi ya viongozi mbalimbali ambazo zinahatarisha usalama wa nchi, lakini waandishi wa habari wengi wao wamekuwa sehemu ya uchochezi huo kwa kwenda kuzitoa habari hizo katika vyombo vyao vya habari bila kuangalia athari zitakazojitokeza baadaye
Bw. Tagalile amesema kutokana na waandishi wengi wa habari kutopenda kusoma vitabu mbalimbali na kujua mambo yatakayowaongezea uelewa, kumesababisha wao kutokujua kama wanaandika habari za kichochezi lakini endapo wataonekana kufanya hivyo kisheria wengi wao wapo kwenye hatari ya kuadhibiwa ikiwemo kufungwa gerezani kwa makosa ya kichochezi waliyoyafanya kupitia habari zao
katika hatua nyingine amewataka waandishi hao wa habari kuacha kujiingiza katika propaganda kwani taaluma hiyo hairuhusu wao kufanya hivyo na badala yake wajikite kuandika habari za kweli zenye manufaa kwa jamii kwani yapo mambo mengi ambayo wanaweza kuisaidia jamii endapo watayaandika kwa kufuata miiko ya taaluma yao
Mafunzo hayo ya siku nne yaliyoanza rasmi jana na yanayotolewa na MCT hii leo yameingia katika siku ya pili mkoani hapo
Na Edwin Moshi