Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa mauaji yaliyofanywa katika mji wa Mpeketoni, Pwani ya Kenya hayakufanywa na kundi la wapiganaji wa kiislamu la Al Shabaab.
Kauli
ya Rais Kenyatta inakuja siku moja baada ya kundi hilo kukiri kufanya
mauaji yaliyotokea Mpeketoni Jumapili usiku na kuua watu zaidi ya
50.
Akitoa hotuba yake ya kitaifa, Rais Kenyatta pia amesema maafisa wa
polisi Mpeketoni ambao walifanya uzembe hadi kutokea mashambulizi hayo
watashtakiwa.
Al Shabaab lilikiri katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa ndilo lilifanya mauaji hayo Jumatatu jioni.
Mauaji zaidi yalifanyika usiku wa kuamkia leo na kuua watu 20 licha ya taarifa ya Al
Shabaab kusema kuwa washambuliaji walioshambulia Mpeketoni walikuwa
wamerejea salama nchini Somalia.
Uharibifu mkubwa ulishuhudiwa katika mji huo huku washambuliaji
wakichoma hoteli na kituo cha polisi pamoja na kuteketeza magari
waliyoyatumia kwa usafiri wao.
Kenyatta amesema kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wanaochochea uhasama miongoni mwa jamii.
