HATIMAYE picha halisi ya gharama ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka
Dar es Salaam (Dart) awamu ya kwanza, imeonesha nauli ya basi kutoka
maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kwenda na kurudi vituo
vikubwa vikiwemo vya Kariakoo na Posta, itapanda kutoka nauli ya chini
ya Sh 400 ya sasa mpaka kati ya Sh 700 na Sh 800 kwa ruti moja.
Kwa wanafunzi, nauli kwa ruti moja kwenda katika vituo hivyo vikubwa
katika mradi huo ambao utaanza kwa majaribio mwishoni mwa mwaka huu,
zitapanda kutoka Sh 200 mpaka nusu ya nauli ya mtu mzima kwa ruti
husika.
Aidha, mfumo wa uendeshaji wa mradi huo na nauli, umewekwa katika
sehemu mbili; sehemu ya kwanza ni usafirishaji wa abiria kutoka maeneo
ya ndani ya makazi ya watu mpaka katika vituo vidogo na vikubwa
vilivyopo barabara kuu za Dart, za Morogoro na Kawawa kwa sasa na sehemu
ya pili ni usafirishaji wa abiria kutoka katika vituo vilivyopo katika
barabara kuu ya Dart za Morogoro na Kawawa, kwenda vituo vikuu vikiwemo
Kariakoo na Posta.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam, katika taarifa ya
mwisho ya Makubaliano ya Dart, iliyotolewa katika mkutano wa Mashauriano
ya Uwekezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo wa Dart.
Mfumo wa nauli
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, abiria atakayelazimika kusafiri na
mabasi ya Dart kwa safari fupi ndani ya barabara zilizo katika makazi ya
watu, kwa mfano wa barabara inayopita Sinza; kutoka Bamaga mpaka
Shekilango, atalipa Sh 500, tofauti na sasa ambapo analipa Sh 400.
Kwa atakayetumia mabasi ya Dart kutoka katika barabara ndogo zilizopo
katika makazi ya watu, kwenda katika vituo vikubwa vya Dart vilivyopo
njia kuu za Morogoro na Kawawa ili kwenda Kariakoo, Posta au Kimara,
atalazimika kukata tiketi ya Sh 800, atakayoitumia kupata usafiri kutoka
barabara ndogo na katika barabara kubwa.
Mfano wa nauli hiyo, ni abiria anayetoka maeneo hayo ya Sinza kwenda
Kimara, Kariakoo au Posta, ambaye atalazimika kukata tiketi ya Sh 800,
itakayomwezesha kupakia basi la Dart kutoka maeneo hayo mpaka
Shekilango, ambako atabadilisha basi kwa tiketi hiyo hiyo, kwenda
Kariakoo, Posta au Kimara.
Aidha kwa abiria watakaolazimika kutumia mabasi matatu ya Dart,
kutoka katika barabara ndogo zilizopo katika makazi ya watu, kupitia
barabara kuu za Dart na kwenda katika eneo lililopo katika barabara
ndogo za makazi ya watu, watalazimika kulipa Sh 900 kwa mabasi yote
matatu.
Aina ya mabasi Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mabasi yatakayotumika
kubeba abiria kwenye njia kuu, yatachukua watu zaidi ya 150 kwa basi
moja, ambapo abiria watakaopata viti vya kuketi ni 52 na wengine
wamewekewa eneo nadhifu la kusimama.
Kwa mabasi yatakayobeba abiria kutoka njia ndogo zilizopo katika
makazi ya watu, yatachukua watu zaidi ya 80, kati ya hao abiria 42 ndio
watakaopata nafasi ya kukaa na waliobakia wamewekewa nafasi nadhifu ya
kusimama.
Foleni, utaratibu
Kuhusu muda utakaotumika kwenye ruti moja ya mabasi hayo ya Dart,
abiria atatumia muda wa dakika zisizozidi 30 kufika anakokwenda,
akitumia mabasi kwenye njia kuu, tofauti na sasa ambapo kwa kutumia
daladala abiria hutumia zaidi ya saa mbili kufika waendako.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini,
utaratibu wa ulipaji nauli kwenye mabasi ya Dart, utakuwa ni wa kutumia
mfumo wa kadi ambapo abiria anatakiwa anunue tiketi kabla ya safari.
“Hakuna kulipa nauli ndani ya basi, abiria anatakiwa alipe kabla ya
kuanza safari, na kama unapanda mabasi matatu, unatakiwa kulipa nauli
yote kwa mara moja kisha unapewa tiketi, unapoingia kwenye basi msomaji
atachukua tiketi yako na kuipitisha kwenye mashine na kupunguza nauli ya
safari hiyo, hadi hatua ya mwisho wa safari,” alisema Sagini.
Alisema utaratibu huo, utapunguza au kuondoa kero kwa abiria na
katika mabasi madogo yanayobeba abiria kuwaunganisha kwenye njia kuu,
yatakuwa na vifaa vya mawasiliano baina ya dereva aliye barabara ndogo
na dereva aliye barabara kuu za Dart.
Tiketi kwa M-Pesa
Kwa mujibu wa Sagini, mradi huo ukianza, abiria watanunua tiketi kwa
kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu kama vile M-pesa, Tigo-pesa,
Pesa Fasta na Airtel Money.
Alisema ili kuzuia wizi na udanganyifu kwenye vituo vya mauzo ya
tiketi na kwenye vituo vya mabasi, zinafungwa kamera na video ili
kuimarisha ulinzi, na kuhakikisha mapato halali kwa ruti zinazofanywa.
“Hii itasaidia kuondoa wizi na uhujumu unaoweza kufanywa katika vituo vya abiria,” alisema Sagini.
Daladala kwaheri
Alisema kwa hatua hiyo, dalaldala za sasa zitaondolewa katika zaidi
ya njia 43 ambazo ziko kwenye barabara ya Morogoro na barabara ya Kawawa
na katika ruti nyingine, daladala hizo zitaendelea kuondolewa hadi hapo
ujenzi wa barabara zote za Dart utakapokamilika.
Katika mabasi hayo ya kubeba abiria kwenye njia kuu za Dart, mabasi
yanayoruhusiwa ni yale yatakayokidhi vigezo, ambavyo ni pamoja na kuwa
na upana wa meta 18 na uwezo wa kubeba abiria 150, ambayo yanahitajika
mabasi 145.
Kwa mabasi yatakayosogeza abiria hadi njia kuu, yatatakiwa yawe na
uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 80 na upana wa meta 12 na yatatakiwa
mabasi 90.
Akitoa mwito kwa wawekezaji wa ndani na nje, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa
Ghasia, alisema ni vyema katika sekta binafsi, wadau wa usafiri na watu
mbalimbali wachangamkie fursa hiyo.
Alisema Serikali kupitia mfumo wa ushirikishaji sekta binafsi, umeona
ni vyema kushirikisha wadau hao kwenye mradi huo mkubwa Afrika
Mashariki, ambao ukitumika vizuri ni chachu ya maendeleo na ukuaji
uchumi.
>>>Habarileo
>>>Habarileo