NAIBU Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Prosper Msofe (48) na
Diwani wa kata ya Levolosi, Ephata Nanyaro (28) jana wamefikishwa katika
Mahakama ya Wilaya ya Arusha/Arumeru, kujibu mashitaka ya shambulio la
kudhuru mwili wa askari mgambo wa Jiji William Mollel.
Akisoma hati ya mashitaka mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Patricia
Kisinda, Wakili wa Serikali, Mary Lucas amedai washitakiwa kwa pamoja,
Aprili 16 mwaka huu, eneo la Levolosi walimshambulia mgambo wa Jiji la
Arusha kwa kumpiga kifuani.
Amedai baada ya kumshambulia wamemsababishia maumivu makali maeneo
mbalimbali ya mwili wake. Washitakiwa wamekana mashitaka na wapo nje kwa
dhamana baada ya kutimiza masharti.
Hakimu Kisinda amesema washitakiwa hawaruhusiwi kutoka nje ya mkoa wa Arusha isipokuwa kwa kibali cha mahakama