Emmanuel Mbasha, ambaye ni mume wa mwimbaji nguli wa nyimbo za
Injili, Flora Mbasha amejitokeza hadharani na kusema kwamba atakwenda
polisi mwenyewe kujibu tuhuma dhidi yake za kumbaka shemeji yake mwenye
umri wa miaka 17.
Faili la tuhuma dhidi ya Mbasha lilifunguliwa Jumatatu iliyopita
katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule) wakati shemejiye huyo
(jina tunalihifadhi), alipotaarifu kuwa Mbasha alimbaka mara tatu kwa
siku mbili tofauti. Kesi hiyo ilipewa namba TBT/RB/3191/2014 na
TBT/IR/1865/2014.
Tangu siku hiyo, polisi imekuwa ikieleza kuwa inamsaka Mbasha bila ya
mafanikio lakini mwishoni mwa wiki mtuhumiwa huyo aliongea na gazeti
hili na kuelezea upande wake wa tukio hilo na kwamba yuko tayari
kujisalimisha ili ukweli ubainike.
“Tuhuma dhidi yangu ni za kutengeneza,” alisema Mbasha na kufafanua
kuwa yote hayo yanatokana na mgogoro wa kifamilia baina yake na Flora na
familia yake ambao alisema umedumu kwa siku kadhaa.
“Mimi sijabaka na sijawahi kubaka; sijatenda dhambi yoyote; sijafanya
kitu chochote na kibaya haya mambo yote ni ya kusingiziwa tu. Mungu
wangu ni shahidi. Na kwa kuwa sijafanya hiyo dhambi kama wanavyodai,
basi Mungu wangu atanitetea,” alisema Mbasha ambaye anaonekana zaidi
kwenye video ya wimbo wa Maisha ya Ndoa alioshirikiana na mkewe Flora.
“Si wamesema wananitafuta, nitakwenda mwenyewe polisi. Nitawasikiliza
na nitatoa maelezo yangu. Kama wakinipeleka mahakamani basi ukweli
utajulikana… ipo siku kila kitu kitakuwa wazi.”
Kabla ya kufunguliwa kwa faili la tuhuma hizo, msichana huyo
alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Ilala (Amana) ambako
alifunguliwa faili la matibabu namba 667. Matokeo ya vipimo ambavyo
vilifanywa na daktari kung’amua kama binti huyo aliingiliwa vinaonyesha
kuwa kulikuwa na mbegu utokaji wa mbegu usio wa kawaida (HVD).
Kadhalika binti huyo alifanyiwa vipimo kuona kama ameambukizwa virusi
vya Ukimwi (VVU), pia kupata ujauzito, lakini matokeo ya awali
yalionyesha kuwa yupo salama.
Akiwa nje ya kituo cha polisi Jumatatu usiku, binti huyo aliliambia
gazeti hili kwamba mara ya kwanza alibakwa mchana Mei 23 na kwamba
mtuhumiwa alirudia kitendo hicho Jumapili Mei 25 usiku ndani ya gari
katika eneo la Tabata, ambako anadai alifanyiwa kitendo hicho mara
mbili.
Hata hivyo, Mbasha alihoji: “Hivi kweli hata kama mimi ni mbakaji,
kweli nimbake mtoto wa kumlea mwenyewe mara tatu, yaani Ijumaa halafu
nirudie tena Jumapili? Hata kama ni kusingiziwa basi tuhuma hizi
zimezidi.”
“Huyu binti nimekaa naye miaka mingi na sijawahi kumfanyia hivyo.
Hapo nyumbani kwangu wamekaa mabinti wengi, wakiwamo shemeji zangu
wadogo zake na Flora na sikuwahi hata kuwagusa, leo hii kwa nini
wananifanyia hivi?”
Mgogoro wa familia
Mbasha alidai kwamba chanzo cha kusingiziwa kwake ni mgogoro baina
yake na mkewe Flora, ambao umesababisha mgawanyiko mkubwa ambao umefanya
achukiwe na familia nzima ya mkewe.
“Yako mambo mengi tu ambayo yanahusu familia, kwa hiyo ilifika mahali
mimi na Flora tukawa hatuishi kwa amani na hata hili jambo limetokea
wakati tukiwa na mgogoro huo.
Hivyo Flora na ndugu zake waliamua
kumlisha binti huyo maneno ili mimi nifungwe,” alisema Mbasha.
Hata hivyo, Flora hakutaka kuingia kwa undani katika suala hilo,
akisisitiza kuwa Mbasha bado ni mumewe na kwamba yaliyotokea awali
alishamsamehe, lakini akamtaka ajitokeze kutoa maelezo polisi.
“Mimi nilishamwambia kwamba hata kama alifanya au hakufanya,
nilishamsamehe kutoka ndani ya moyo wangu maana yeye ni mume wangu wa
ndoa na Mungu wangu ni shahidi, lakini kuna suala la kisheria polisi
ambalo mimi siwezi kuliingilia,” alisema Flora ambaye alitamba na wimbo
wa injili wa “Tanzania” ambao ulimfanya aalikwe katika shughuli mbalimba
za kitaifa.
“Tatizo linakuwa kubwa kwa sababu yeye mwenyewe haonekani na taarifa
ni kwamba amekimbia,” alidai Flora. “Sasa kama kweli hajafanya kitendo
hicho, kwa nini anajificha? Ajitokeze… aende polisi na huko ndiko akatoe
maelezo yake. Kuzungumza na vyombo vya habari haisaidii kabisa.”
Mwimbaji huyo, ambaye ni mjukuu wa muhibiri maarufu wa Injili, Askofu
Moses Kulola alisema yeye hana uwezo wa kuingilia kesi hiyo kwani
hakuhusika kwa namna yoyote ile kupeleka suala hilo polisi kwa sababu
hakuwapo wakati likitokea na kwamba linasimamiwa na familia.
“Inawezekana anatamani nikafute kesi polisi, mimi sina uwezo huo kwa
sababu ni suala la kisheria na tuhuma zenyewe ni za kijinai. Pili
familia yenye mtoto ndiyo inafuatilia kesi hiyo, lakini hilo halifuti
msamaha wangu kwake,” alisisitiza.
Kauli ya Flora kwamba ameshamsamehe mumewe inafanana na ya Mbasha
ambaye pia alisema kwamba kama kuna jambo ambalo mkewe alimkosea, hana
tatizo na kwamba alishamsamehe.
“Flora ni mke wangu, mke wa ujana wangu, ninampenda asilimia 100 na
yeye analifahamu hilo, lakini sijui ni kitu gani kimemkuta? Sijui ni
nini kimeingilia ndoa yetu?” alihoji Mbasha.
Alisema ameshampigia simu mkewe mara nne akitaka waonane ili
wazungumze, lakini hakuonyesha utayari, kauli ambayo Flora aliikanusha
akisema: “Hajanitafuta maana tangu Jumatatu hapatikani kwenye simu.”
Mwenendo wa upelelezi
Wakati hayo yakiendelea, maendeleon ya kesi hiyo yanasuasua baada ya
faili kutokupelekwa Kituo cha Polisi Buguruni kutoka Tabata kwa ajili ya
hatua zaidi.
Baadhi ya wanafamilia wa mtoto anayedaiwa kubakwa walisema jalada
hilo lingefikishwa Buguruni Jumatano jioni, lakini kutokana na ofisa
anayeshughulikia kesi hiyo kuwa na udhuru, ilishindikana.
Mjomba wa Flora ambaye amepewa jukumu la kusimamia kesi hiyo, alisema
wamekuwa wakifuatilia Kituo cha Polisi cha Tabata tangu tukio hilo
liliporipotiwa, lakini wakaelezwa kuwa kesi hiyo itahamishiwa Buguruni.
“Tuliambiwa lile faili lazima lihamie kituo cha Buguruni. Nilifika
hapa nikaonana na kamanda wa polisi wa wilaya ambaye ametupokea vizuri
na kuonyesha moyo wa kutusaidia,” alisema.
Kamanda wa polisi wa Ilala, Marietha Minangi alisema bado wanaendelea
na uchunguzi wa kesi hiyo na kwamba hafahamu taarifa kuwa faili hilo
linacheleweshwa kuhamishiwa Buguruni. “Tunaendelea kuchunguza, ila
siyajui hayo masuala ya faili yanayotoka kinywani mwako. Lakini nimepata
taarifa kuwa bado wanachunguza,” alisema Minangi.
Mwanzoni mwa wiki jana, Kamanda Minangi alisema kuwa maofisa wake
walikuwa wanaendelea kumsaka mtuhumiwa na kwambawalienda mpaka nyumbani
kwake, lakini hawakumkuta.
“Nimefuatilia ni kweli hiyo kesi imefunguliwa na maofisa wangu
wameniambia walienda nyumbani kwake na hawakumkuta mtu. Waliniambia
walikaa pale kwa takribani dakika 20 na ile nyumba ina fence (uzio) na
geti waligonga kengele, lakini hakuna mtu aliyekuja kufungua.
“Na baadaye waliwauliza majirani, nao wakasema hawafahamu mtu huyo
alipo. Inaonekana ametoweka, lakini sisi kama wasimamizi wa sheria
tunaendelea kumtafuta mpaka tutakapomkamata,” alisema Minangi.
Ustawi wa Jamii
Kesi hiyo pia inafuatiliwa kwa karibu na Idara ya Ustawi wa Jamii ya
Manispaa ya Ilala kujua usalama na matibabu ya binti huyo.
Ofisa ustawi
wa jamii anayeshughulikia ulinzi na usalama kwa mtoto wa manispaa hiyo,
Fransica Makoye alisema kuwa wanalishughulikia suala hilo kama mengine
katika kutafuta haki na usalama wa mtoto na wala hawahusishi na umaarufu
wa wahusika.
“Sisi tunafuatilia kama alipata tiba sahihi mara baada ya tukio la
kubakwa na kufahamu mahali ambako anakaa kwa ajili ya usalama wa huyo
mtoto. Tumeiona PF3 haionyeshi kama alipata matibabu, lakini
tutawajulisha zaidi kinachojiri kwa kuwa tutaenda Hospitali ya Amana kwa
maelezo zaidi,” alisema Makoye.
Chanzo: Mwananchi