Msiba wa mtoto Nasra Mvungi (4),
aliyeteswa kwa kufungiwa katika boksi kwa miaka minne, ambako ndiko
alikokuwa akipewa chakula, kwenda haja kubwa na ndogo na kulala, imeibua
simanzi jijini Dar es Salaam, Morogoro na katika maeneo mbalimbali nchini.
Jana
taarifa za kufariki kwa Nasra aliyekuwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, zilisambaa katika maeneo mbalimbali
nchini na baadaye kuthibitishwa na Msemaji wa
hospitali hiyo, Aminiel Aligaeshi.
Mwishoni
mwa wiki, mama mlezi wa Nasra, Josephina Joel, alisema hali ya mtoto huyo
ilibadilika ghafla Mei 21 jioni, hali iliyosababisha madaktari waliokuwa zamu
kumwekea mashine ya kumsaidia kupumua, ambayo alikuwa akiitumia mpaka karibu na
mwisho wa maisha yake.
Akizungumza
na mwandishi jana, Ofisa Ustawi wa Jamii mkoani Morogoro, Oswin Ngungamtitu,
alisema kuwa mwili wa Nasra utasafirishwa leo kutoka Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kwenda Morogoro na taratibu
zote za maziko zitafanywa na Ofisi ya Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Jeshi
la Polisi.
Ngungamtitu
alisema kuwa kabla ya maziko, Nasra ataswaliwa katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro badala ya nyumbani kwa mzazi wake, kwa kuwa baba mzazi wa mtoto huyo,
Rashid Mvungi, ni mmoja kati ya washitakiwa wa kesi iliyofunguliwa mahakamani
ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
Aidha
taarifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, John Laswai, alieleza kuwa
taratibu za kipolisi zitafanywa ikiwa ni pamoja na kupata taarifa ya daktari
itakayoeleza sababu za kifo cha mtoto huyo.
Taarifa
hiyo kwa mujibu wa Kamanda Laswai, itapelekwa kwa wanasheria ambao wataipitia
na kama itaonesha kuwa kifo cha Nasra kimetokana na ukatili na washitakiwa,
basi Mvungi ambaye yuko nje kwa dhamana, atakamatwa na kesi itabadilika.
Tayari
Mkurugenzi wa Kampuni ya mabasi ya Al Saed, Omary Al Saed, amejitolea usafiri
wa kwenda Dar es Salaam kuchukua mwili na kuurudisha mkoani Morogoro kwa maziko
na fedha taslimu Sh 400,000, kwa ajili ya gharama za dawa za kuhifadhi mwili
pamoja na sanda.
Hata
hivyo hatua ya Serikali kuamua swala kufanyika katika Uwanja wa Jamhuri,
haikumfurahisha baba wa marehemu, ambaye katika
kikao cha maandalizi ya maziko, alidai angefurahi kama angepewa mwili wa
mtoto wake ili amzike mwenyewe badala ya kuzikwa na Serikali.
Mvungi
alidai taarifa za kufariki kwa mtoto wake huyo zimemchanganya na hajui
cha kufanya, kwa kuwa tayari alishakaa na familia yake akiwemo mke wake na
kukubaliana kumlea Nasra.
Katika
makubaliano hayo kwa mujibu wa madai ya Mvungi, walikuwa wakisubiri apone ili
wapeleke maombi Ofisi ya Ustawi wa Jamii, wapate ruhusa ya kumlea Nasra.
Alidai
kuwa hakutarajia kwamba ndoto yake ya kumlea mtoto huyo tangu abainike kuishi
kwa mateso katika boksi kwa zaidi ya miaka mitatu, ingeishia hapo lakini kwa
mapenzi ya Mungu imetokea hivyo hana njia ya kuzuia.
Nasra alihamishiwa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili Jumatano iliyopita kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro, kwa ajili ya uchunguzi na tiba zaidi.
Mama mlezi wa mtoto huyo hospitalini
hapo, Josephine alisema: "Nimesikitishwa
sana, lakini ni Mungu ameamua kufanya kazi yake na hakuna anayeweza kupangua."
Msiba huo umetokea wakati Juni 9 mwaka huu katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi mjini Morogoro, Mvungi na washitakiwa wenzake wakitarajiwa
kufikishwa mahakamani hapo kujibu mashitaka ya kula njama na kufanya ukatili
dhidi ya Nasra.
Washitakiwa wenzake Mvungi ni aliyekuwa mama mlezi wa Nasra,
Mariamu Said (38) na mume wake, Mtonga Omar (30).
Washtakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo Jumatatu
iliyopita chini ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Mary Moyo na kusomewa mashtaka hayo.
Wakili wa Serikali, Sunday Hyera alidai kuwa washitakiwa
walitenda makosa hayo ya ukatili kati ya
Desemba 2010 na Mei mwaka huu, katika mtaa wa Azimio Kata ya Kiwanja cha Ndege,
mjini Morogoro.
Wakili huyo alidai kuwa katika wakati huo, washtakiwa wakiwa
walezi wa mtoto Nasra, walimfanyia ukatili wa kumtelekeza na kumpa malezi akiwa
ndani ya boksi na kumsababishia magonjwa.
Wakili huyo wa Serikali, alitaja maradhi yaliyomkumba mtoto
huyo akiwa ndani ya boksi kuwa ni pamoja na utapiamlo, maumivu ya kifua na
mvunjiko wa mifupa katika mwili wake.
Hyera alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na
kuiomba Mahakama kutaja tarehe ya kuisikiliza.