Maafisa wa polisi wa Kenya wamemtia nguvuni mshukiwa anayetuhumiwa
kuendesha akaunti ya Twitter ambayo ina uhusiano na kundi la kigaidi la
Al shabaab na uliotoa habari kwamba Al shabaab walihusika kutekeleza
mauaji eneo la Mpeketoni kaunti ya Lamu.
Kwa mujibu wa Ripota Julius Kepkoech toka Kenya, Katibu wa
wizara ya Mambo ya ndani na usalama wa taifa, Mutea Iringo
amethibitisha kwamba Ismail Omondi ametiwa nguvuni Tarehe 18 June mwaka
huu ambapo hata hivyo Iringo amekanusha kwamba mshukiwa huyo hana
uhusiano wowote na Al Shabaab.
Iringo amesema, “Unaweza kuona kwamba yule anayekiri kuhusika na Alshabaab si mmoja wa kiongozi wa kundi hilo,”.
Inspekta Jenerali wa Polisi David Kimaiyo awali alisema kupitia
ukurasa wake wa Twitter kwamba: “Aliye kizuizini kwa sasa ni mshukiwa
anayeendesha mtandao wa kijamii unaodhaniwa kutumiwa na Al shabaab
kukiri kuhusika na uvamizi”
Hata hivyo Kimaiyo hakutoa taarifa zaidi kuhusiana na washukiwa.
Ismail Omondi ni mshukiwa wa tatu kutiwa nguvuni kuhusiana na mauaji
yaliyotokea Mpeketoni siku ya Jumapili na Jumatatu ambapo zaidi ya watu
60 wamepoteza maisha.
Mapema siku ya Jumatano, mshukiwa mwingine Ahmed Abdallah
anayetuhumiwa kumiliki gari lililowabeba wavamizi hao alikamatwa huku
Salim Dyana naye akikamatwa na polisi kwa tuhuma za kuliendesha gari
lililowabeba wavamizi kuelekea Mpeketoni Lamu.
