Mark Mwarabu, dereva aliyekuwa akimwendesha sista wa Kanisa
Katoliki, Crecensia Kapuri aliyeuawa na majambazi wa Kanisa Katoliki,
amesema mbinu za kijeshi zilimwokoa katika tukio hilo.
Katika tukio hilo, Sista Kapuri kutoka Parokia ya
Gaudence-Makoka na ambaye alikuwa mhasibu wa Shule ya Sekondari
Mwenyeheri Anuarite kutoka Shirika la Bikira Maria Malkia wa Mitume,
aliuawa na majambazi Juni 24 mwaka huu eneo la Riverside, Ubungo jijini
hapa alipokuwa akifanya ununuzi katika moja ya duka la chakula.
Akisimulia mkasa huo muda mfupi baada ya
kumalizika kwa misa ya kuuaga mwili wa sista huyo tayari kwa safari ya
kwenda mkoani Mbeya kwa maziko yatakayofanyika kesho, alisema majambazi
hao walipofika hawakuzungumza na mtu bali walifyatua risasi.
“Hawakuzungumza chochote na sisi bali nilisikia
mlio wa risasi pekee na kwa kuwa mimi nilikuwa mwanajeshi, nilijua moja
kwa moja kuwa hizo ni risasi na nikawaeleza laleni chini (wakiwa ndani
ya gari) ili zisiwafike,” alisema.
“Niliposikia hivyo, nilikunja usukani kurudisha
gari nyuma wakati huo risasi ziliendelea kufyatuliwa kulenga gari letu
na zilikuwa zikitoka katika gari lililokuwa limeegeshwa likishusha
mizigo,” alisema Mwarabu aliyedai alistaafu Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) mwaka 1989.
Aliongeza: “Sista aliyekuwa nyuma alifungua mlango
na kukimbia ndipo mimi nilipopigwa risasi tatu kwenye mkono wa kulia,
mbili zilikata kidole gumba na moja ilinijeruhi kidole cha pete na sasa
mkono mzima una ganzi.
“Niliinama kukwepa risasi hizo kwani walikuwa na
lengo la kuukata mkono mzima lakini nilikuwa nikikwepa na kuendesha kwa
makini na ndipo wakanijeruhi vidole. Namshukuru Mungu kwa kuninusuru.”
Mwarabu alisema wakati majambazi hao wanapiga
risasi bila mpangilio, risasi kadhaa zilimpata sista huyo aliyekuwa
amebaki ndani ya gari na kupoteza maisha palepale.
Alisema baada ya hapo wasamaria wema walimuwahishwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu na mwili wake ulipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Alisema baada ya hapo wasamaria wema walimuwahishwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu na mwili wake ulipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kuhusu utata wa fedha zilizoibwa, alisema asingeweza kulizungumzia suala hilo kwa kuwa yeye ni dereva tu.
Juzi Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleimani Kova alisema fedha zilizoibwa ni Sh20 milioni.
Askofu aelezea kifo
Akihutubia mamia ya waumini waliojitokeza kutoa
heshima za mwisho, Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Gerevas Nyaisonga
alisema kifo cha Sista Kapuri ni cha kuhuzunisha kutokana na aina ya
mauaji aliyofanyiwa.
“Yanayotokea leo matukio kama haya... kwa kuua hatuwezi kuondoa
ugumu wa maisha yetu, kwa kuua hatuwezi kuboresha maisha yetu wala
kuleta amani,” alisema askofu.
“Sista amefariki, anakwenda kuzikwa na kutuachia
maswali magumu yasiyokuwa na majibu. Ukali wa maumivu na mateso
angetueleza ni nani aliyetenda hayo,” alisema Askofu Nyaisonga.
Akitoa wasifu mfupi wa marehemu, Mama Mkuu wa
Shirika la Bikira Maria Malkia wa Mitume alisema, Sista Kapuri alizaliwa
Agosti 29, 1962 na alifunga nadhili zake mwaka 1980.
Naye askofu msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar
es Salaam, Titus Mdoe akitoa salamu za pole za jimbo hilo na za Baraza
la Maaskofu Tanzania (TEC), alisema kifo kimetokea hakuna budi
kukipokea.
“Watawa hawa hawana kitu chochote kwani wametoa
maisha yao kuitumikia jamii. Ukimwona sista amebeba fuko la fedha siyo
lake ni kwa ajili ya kuwahudumia watu.”
Kwa kuwa alikuwa mlezi wa watoto wetu wa taifa la
kesho, alikwenda kuwatafutia chakula watoto wake na hao walikuwa
wakimsubiri mama yao kuona atakuja na nini, lakini ndiyo hayo
yaliyotokea,” alisema Mdoe.
Naye kaimu mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond
Moshi alisema Serikali itahakikisha inawatia nguvuni wale wote ambao
walijihusisha na tukio hilo. Mushi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya
Ilala, alisema: “Juhudi siyo kuwapata bali ni kuzuia matukio ya aina hii
na tunaomba ushirikiano katika kuwabaini wanaofanya vitendo vya aina
hii.”
>>>MWANANCHI
>>>MWANANCHI