Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Alsaed, Omary Al Saed wa mjini
Morogoro anakusudia kuwasiliana na wadau wenzake ili kuanzisha Taasisi
ya Nasra Mvungi Foundation, ili kuonyesha namna walivyoguswa na mateso
na hatimaye kifo cha mtoto huyo aliyefichwa kwenye boksi kwa muda wa
miaka mitatu.
Mtoto huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni mosi mwaka huu,
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam alikokuwa
amelezwa kwa matibabu ya nemonia.
Nasra ambaye kifo chake kimewagusa watu wengi ndani na nje ya Mkoa wa
Morogoro, alizikwa juzi katika makaburi ya Kola mjini hapa.
Akizungumza na gazeti hilo jana, Al Saed alisema amehuzunishwa na
mateso na hatimaye kifo cha mtoto huyo na kwamba, ili kuonyesha kuwa
ameguswa, ameamua kuwasiliana na wadau wengine ili waone uwezekano wa
kuanzisha mfuko huo.
Alisema mfuko huo pia utatumika kuwasaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na wenye mahitaji muhimu.
Alisema hiyo ni njia nzuri ya kukumbuka kifo cha mtoto Nasrah na maisha aliyoishi wakati wa uhai wake.
Mkurugenzi huyo pia alisema atajenga kaburi la mtoto huyo ili iwe kumbukumbu ya kudumu kwa watu wa familia yake na jamii kwa ujumla.
Alsaed alisema ujenzi wa kaburi hilo utafanyika mwishoni mwa wiki hii kwa kutumia marumaru.
Wakati huo huo, Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali mkoani Morogoro,
Sunday Hyera amesema hajui chochote kuhusu namna kesi inayowakabili watu
wanaotuhumiwa kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo
itakavyo kuwa.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mariamu Said ambaye ni mama mkubwa wa
Nasrah, baba yake mzazi Rashidi Mvungi na mume wa Mariamu, Omary Mtonga.
Chanzo: Mwananchi.
