WIZI NA UHARIBIFU MKUBWA WATOKEA KWENYE SOKO LA NGIU WILAYANI MAKETE

Katika hali ya kusikitisha na kushangaza pia, watu wasiofahamika wameiba miundombinu pamoja na kufanya uharibifu katika soko la wakulima la Ngiu lililopo kata ya Iwawa wilayani Makete mkoani Njombe licha ya soko hilo kulindwa na mlinzi

Mwandishi wa mtandao huu ambaye amefika eneo la tukio baada ya kupenyezewa taarifa na watumiaji wa soko hilo pia ameshuhudia uharibifu uliofanywa na watu wasio wahamika ambao wamegeuza kuta za majengo ya soko hilo kuwa ubao wa darasani kwa kuandika na kuchorachora kwa kutumia mkaa

Miundombinu iliyoibiwa sokini hapo ni pamoja na mifuniko yote ya chuma ya kufunikia masinki ya chemba za vyoo sokoni hapo ambayo yapo nyuma ya soko pamoja na baadhi ya mabomba ya kutititishia maji ya mvua kutoka kwenye paa hadi chini ili yatiririke kwa mpangilio maalumu

Inasadikika kuwa matukio hayo ya wizi yamekuwa yakitendeka kwa nyakati tofauti na ndiyo maana imekuwa si rahisi kwa watu kufahamu kuhusu wizi huo, hadi Jumatano ya wiki hii kulipokuwa kukifanyika mnada sokoni hapo ndipo wananchi waliposhtuka kuona vifaa hivyo vimeibwa
Chemba ipo wazi, mfuniko umeibwa.
Akizungumza na mtandao huu mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Sulemongo wa Mongo amesema soko hilo lilijengwa na serikali kwa gharama kubwa na kutokana na tukio hilo la wizi limetia dosari wilaya ya Makete hivyo mlinzi wa soko hilo anatakiwa kuwa wa kwanza kukamatwa na kujibu tuhuma hizo

"Mwandishi ni fedha nyingi zimetumika kujenga soko hili, sasa nashangaa watu hao wasiopenda maendeleo wanakuja kuiba hapa sokoni inamaana mlizi alikuwa wapi? au kunamaana gani ya kuweka mlinzi? na inaonesha wanakujaga kuiba kidogo kidogo hao wezi hawakuja kuiba vitu vyote hivi kwa siku moja" alisema Sulemongo

Pia kuta za majengo ya soko hilo ambalo lipo kandokando ya barabara ya makete-njombe, zimechafuliwa kwa kuchorwa chorwa picha mbalimbali na maandishi ya maneno ambayo hayaeleweki
Kuta zikiwa zimechorwa na kuandikwa andikwa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa soko hilo Bw. Tuko Sanga akizungumzia sakata hilo, amesema ulizi wa soko hilo ni tatizo na ndiyo maana wizi huo umetokea na yeye kama mwenyekiti tayari ameshatoa taarifa kwa uongozi wa juu (Idara ya kilimo Makete) kwa hatua zaidi

Amesema ana miezi miwili ama mitatu hajawahi kumuona mlizi huyo jambo linaloashiria kuwa ukosefu wake huo wa kutokuwepo kwenye kituo chake cha kazi huwenda kumesababisha wezi kutumia nafasi hiyo kuiba miundombinu hiyo ya soko

Bw. Sanga amesema baada ya kuona hali hiyo imejitokeza yapo mabomba mawili yaliyokuwa yamelegea na wamelazimika kuyatoa na kuyaingiza ofisini kwa kuogopa kuwa yataweza kuibiwa kirahisi, huku akitupa lawama kwa wanafunzi wa shule moja ya msingi (jina tunalo) kuwa ndio wamekuwa wakiandika na kuchora kwenye kuta za soko hilo na wameshatoa taarifa kwa waalimu wao.
 Bomba linaopitisha maji ya mvua likiwa limeibwa.
Mwandishi wetu aliwasiliana kwa njia ya simu na afisa kilimo, mifugo na ushirika wa halmashauri ya wilaya ya Makete kutaka kufahamu ni hatua gani wamechukua juu ya sakata hilo lakini hadi tunatoa habari hii simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa licha ya tetesi kuwa yupo nje ya wilaya kikazi

Pia jitihada za kumtafuta mlinzi wa soko hilo zinaendelea

Soko la Ngiu hutumika mara moja kwa kila mwezi kuuza bidhaa mbalimbali likijumuisha wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya wilaya ya Makete

Habari/picha na Edwin Moshi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo