CHAMA cha wauguzi nchini tawi la mkoa wa Dodoma, kimeitaka Serikali
kukabiliana na tatizo la wahudumu feki ambao wanagushi vyeti na
kujihusisha na huduma hiyo.
Wauguzi hao, wametoa kilio cha leo Mei 16, 2014 wakati wakiongea, kwa masharti ya kutotajwa majina yao mtandaoni (majina tunayo)
ambapo wamesema katika baadhi ya Hospitali na Zahanati zilizopo mkoani
humo wapo baadhi ya wauguzi wasio na taaluma ya fani hiyo, na kulazimika
kuitaka Serikali kuwa na mkakati wa kufanya ukaguzi wa wahudumu na
wauguzi ili kuondoa wauguzi wa aina hiyo.
Aidha, wamesema hali hiyo inachangia
kuwepo kwa lawama kutoka kwa wagonjwa kwa huduma wanazopatiwa na
wauguzi wa aina hiyo, kutokana na kukosa maadili ya kazi hiyo.
“Wakija hata leo wakikagua watawakamata watu wengi ambao hawajasomea katika fani hii, sisi tunaishauri serikali kuchukua hatua za haraka ili waweze kujua kuwa wanahujumiwa,” alisema mmoja wa wauguzi hao.
Hata hivyo, wamesema tatizo la
ukosefu wa vifaa vya kutendea kazi katika maeneo yao, umesababisha jamii
wanayoihudumia kutokuwa na imani nayo pale wanapo lazimika kuwaambiwa
wagonjwa kuwa wakanunue vifaa tiba na dawa kwenye maduka ya dawa baridi.
na FIKRAPEVU