OFISI za gazeti la Daraja Letu zilizopo eneo la Uwanja wa Ndege mjini
Njombe, zimevunjwa na kuibwa nyaraka muhimu mbalimbali na kompyuta tano.
Akizungumzia wizi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Daraja ambalo
ni wachapishaji wa gazeti hilo, Simon Mkina (Pichani) alisema wizi huo uliotokea
usiku wa Aprili 30, 2014.
Alisema kufuatia wizi huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linawashikilia
watu wawili kwa uchunguzi zaidi.
Mkina akizungumzia mazingira ya wizi huo, alisema dalili zinaonesha kuwa
ulipangwa ama na baadhi ya watu wanaojua vyema taratibu za kazi za
shirika lake, au watu wenye uhusiano wa karibu na ofisi hiyo.
"Kuna uwezekano mkubwa wa kuhusika kwa watu wa karibu na shirika letu,
lakini kwa kuwa tayari Polisi imeanza kazi zake, ni vyema tukaliacha
jeshi hilo likaendelea na matokeo yake tutaambiwa," aliongeza Mkina.
Mkurugenzi huyo pia alisema huenda asili ya kazi za gazeti lao, hasa
habari za uchunguzi ikawa sababu nyingine ya wahusika wa wizi huo wa
nyaraka kuhusika.
"Siwezi kueleza moja kwa moja iwapo habari zetu za uchunguzi zikawa
chanzo pia, lakini sio chanzo cha kupuuza, maana utendaji wetu umekuwa
mwiba kwa waendaji wabovu wa halmashauri," alisema Mkina.
Gazeti la Daraja Letu limekuwa likiandika habari za utendaji
usioridhisha wa baadhi ya viongozi wa halmashauri za mikoa ya Njombe na
Iringa. kufuatilia matumizi ya fedha na pia kuibua changamoto za maisha
na maendeleo kwa mikoa hiyo miwili.