Mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Ester Shaban (44) amejikuta
akirudia machungu ya kufiwa na mume wake kwa kufiwa na watoto wa kuwazaa
kutokana na kuumwa na mbwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Ester alifika Kibamba-Kwembe, nje kidogo
ya Jiji la Dar na watoto wake watatu akitokea Kahama, Shinyanga ili
kupumzika kwa ndugu yake baada ya kufiwa na mume wake miezi kumi na nne
iliyopita.
Siku ya pili tangu afike watoto wake, Boniface Joseph (4) na Peter Joseph (6) waling’atwa na mbwa sehemu za usoni.
Tukio hilo lilitokea wakati mama yao amekwenda Makondeko, Dar na kuwaacha watoto hao nyumbani bila kuwepo kwa mtu mzima.
Chanzo kilisema mwanamke huyo alirudi saa mbili usiku na kukutana na
mkasa huo wa watoto wake kung’atwa na mbwa, wakiwa na majeraha usoni.
“Mtoto mmoja aliyeshuhudia tukio hilo alisema watoto hao ndugu
waling’atwa usoni na mbwa wa mzee mmoja ambaye hata yeye alimkimbiza
mchana,” kilisema chanzo hicho.
Naye mama wa mtoto huyo akizungumza na Risasi Mchanganyiko kwa
masikitiko, alisema: “Baada ya kukuta wanangu wamekumbwa na mkasa huo
niliwachukua mpaka kwa mwenye mbwa na kumweleza lakini akakataa kwamba
si mbwa wake japokuwa alionekana kuwa na kigugumizi cha hapa na pale.”
Akaongeza: “Tulishauriana tuwapeleke Hospitali ya Tumbi (Kibaha)
lakini yule mzee aliyesemekana kuwa ndiye mwenye mbwa akasema yeye hana
pesa za kukodi gari labda tusubiri Jumatatu. Siku hiyo ilikuwa Jumamosi
tena saa tatu usiku.
“Nilipinga, ikabidi kesho yake (Jumapili) tuwapeleke hospitali ya binafsi ya Gati ambapo walichomwa sindano za tetenasi tu.
“Niliwauliza madaktari kama sindano hizo zinatosha wakasema zinatosha
kwani chanjo niliyoipata mimi wakati wa ujauzito itawasaidia na watoto.
Nilishangaa kwa sababu nasikia mtu akiumwa na mbwa anachomwa sindano za
kitovuni lakini wanangu hawakufanyiwa hivyo.”
Mwanamke huyo aliendelea kudai kuwa daktari alimtoa wasiwasi kwa
kumwambia vidonda hivyo vitapona asiwe na shaka. Akapewa dawa za kumeza
watoto wake na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Akasema: “Baada ya siku kadhaa, vidonda vilionekana kukauka kwa nje, Kumbe sikujua kwa ndani watoto wangu walikuwa wanaumia pasipo kufahamu. Siku chache mbele Peter akazidiwa.
Akasema: “Baada ya siku kadhaa, vidonda vilionekana kukauka kwa nje, Kumbe sikujua kwa ndani watoto wangu walikuwa wanaumia pasipo kufahamu. Siku chache mbele Peter akazidiwa.
Akawa anatapika damu na kubweka kama mbwa. Ila sikujua cha kufanya, kwa kuwa ilikuwa usiku nilivumilia.
“Ilipofika alifajiri ya saa 10 mwanangu alikata roho. Tulipeleka mwili kwenye mochwari ya Tumbi kwa ajili ya kuuhifadhi.
“Siku iliyofuata tukiwa mochwari tunauchukua mwili, tulimsimulia
daktari ugonjwa uliomuua mwanangu akasema tumpeleke Boniface (mwanaye
mwingine) ili afanyiwe matibabu. Kumbe kule nyumbani Boniface naye
alikuwa amezidiwa na yuko njiani wanamleta hospitali. Alipofikishwa tu
hakukaa sana akafariki dunia,” alisema mwanamke huyo.Mwanamke huyo akaendelea kusema kufiwa kwa watoto wake hao ni pengo
kubwa sana katika maisha yake kwani kwa sasa amebaki na mtoto mmoja
ambaye ni wa mgongoni.
“Moyo unaniuma sana ila sina namna zaidi ya kumshukuru Mungu kwa
yote. Nilikuja kupumzika na watoto wangu hapa baada ya kifo cha baba
yao, sasa siku nikirudi Kahama nitakuwa peke yangu,” alisema mama huyo
na kuanza kulia.
Mwanamke huyo pia alisema anawaomba wasamaria wema wamsaidie kwa hali
na mali kwani kwa sasa ni mjane na anahitaji kurudi Kahama ili kupeleka
msiba wa watoto wake.
Kwa yeyote mwenye kuguswa na matatizo ya mama huyu anaweza kumsaidia kwa namba 0767 449758, jina litasoma Stella Shaban.
Marehemu hao walizikwa katika Makaburi ya Kibamba, Dar kwa kupishana siku moja. Mungu azilaze pema peponi roho zao. Amina.
>>>>GPL