UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa hoja kwamba, kutokana na Taarifa zilizowasilishwa katika Bunge
lako Tukufu na Wenyeviti wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati
ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Kamati ya Uchumi, Viwanda na
Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya
Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na Mwelekeo kwa
Mwaka 2014/2015. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha
Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake
pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2014/2015.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote na kwa masikitiko makubwa naomba nichukue fursa hii kutoa salamu za pole kwako na kwa Bunge
lako Tukufu kwa kuondokewa na wabunge wawili, Mheshimiwa William
Augustao Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa Kalenga, aliyefariki tarehe 01
Januari, 2014 na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge
wa Chalinze, ambaye alifariki tarehe 22 Januari 2014. Aidha, niwape
pole Wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kifo cha Mheshimiwa John Gabriel Tupa
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, kilichotokea tarehe 25 Machi 2014, na kwa
Wananchi wa Wilaya ya Urambo kwa kifo cha Mheshimiwa Anna Magowa
aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, kilichotokea tarehe 24 Septemba 2013.
Vilevile, natoa pole kwa Wananchi wa Wilaya ya Kalambo kwa kifo cha
Mheshimiwa Moshi Mussa Chang’a aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo,
aliyefariki tarehe 21 Aprili 2014. Naomba pia niwape pole Waheshimiwa
Wabunge na Wananchi wote waliofiwa na ndugu na jamaa zao kutokana na
majanga na matukio mbalimbali tangu nilipowasilisha Bajeti yangu ya
mwaka 2013/2014.
Tunamwomba
Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina!
Nichukue fursa hii pia kuwapa pole Wahanga wote wa majanga mbalimbali
yakiwemo mafuriko na ajali za barabarani, na niwashukuru kwa dhati wote
waliotoa misaada ya hali na mali wakati wa ajali na maafa hayo.
3. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha 2013/2014, Bunge lako Tukufu limepata Wabunge wapya watatu
ambao ni Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani; Mheshimiwa
Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya
Kikwete, Mbunge wa Chalinze. Nawapongeza kwa kuchaguliwa kuwawakilisha
Wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawaomba
watumie fursa waliyoipata kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
MAANDALIZI YA BAJETI
4. Mheshimiwa Spika,
huu ni mwaka wa pili tangu tuanze utaratibu wa Mzunguko mpya wa Bajeti
ambao unatuwezesha kukamilisha Mjadala wa Bajeti ya Serikali ifikapo
tarehe 30 Juni ya kila mwaka. Taarifa za awali zinabaini kwamba
utaratibu huu umeanza kuonesha mafanikio ya haraka katika utekelezaji wa
kazi zilizopangwa. Bajeti hii imeendelea kutayarishwa kwa
kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi ya mwaka 2010; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi
na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Mpango wa Kwanza wa
Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2011/12 hadi 2015/16; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; na Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now – BRN).
Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya
kipaumbele iliyoainishwa kwenye mipango hiyo ya Kitaifa ili kuleta
maendeleo endelevu na ya haraka yatakayowanufaisha Wananchi wa
Tanzania.
5. Mheshimiwa Spika,
nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa
mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi waliyoifanya ni kubwa na ambayo
imetuwezesha kukamilisha maandalizi ya Bajeti ninayoiwasilisha leo.
Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa kukamilisha mjadala wa
Bajeti ya Serikali na utekelezaji wake.
HALI YA SIASA
6. Mheshimiwa Spika, kwa
ujumla hali ya siasa Nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa vinaendelea
kutekeleza majukumu yao. Nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mpito
ambapo tunaandika Katiba Mpya itakayoweka mustakabali wa mwelekeo wa
Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Nawasihi Wanasiasa na Wananchi wote
kwa ujumla kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa maandalizi ya Katiba hiyo
ambayo baadaye wananchi wote wataipigia kura ya maoni. Nawaomba
tushindane kwa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu katika kuandaa Katiba
hii ambayo itatuongoza sasa na vizazi vijavyo.
7. Mheshimiwa Spika, katika
jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi Nchini,
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeratibu shughuli za Vyama vya
Siasa kwa kuhakikisha kunakuwepo na fursa sawa katika shughuli za siasa
Nchini. Hadi Aprili 2014, idadi ya Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa
kudumu imefikia 21 baada ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kupata
usajili wa kudumu mwezi Juni, 2013. Aidha, Chama cha Alliance for Change
and Transparency (ACT-TANZANIA), Chama cha Wananchi na Demokrasia
(CHAWADE) na Chama cha Maridhiano na Uwiano (CMU) vimepata usajili wa
muda. Nirejee wito wangu kwa Viongozi na Wanachama wa vyama vyote vya
siasa kuendeleza utamaduni wa kuvumiliana na kutohamasisha siasa za
chuki na vurugu ambazo zinaweza kutugawa na kuhatarisha amani, utulivu
na umoja wa Taifa letu tulioujenga kwa miaka mingi.
ULINZI NA USALAMA
Usalama wa Raia
8. Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu imeendelea kudumisha amani na utulivu kama tunu ya Taifa
iliyojengwa na kuimarishwa tangu tulipopata uhuru. Katika mwaka
2013/2014, Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza Programu ya Maboresho
ya Jeshi na Mkakati wa Kupunguza Uhalifu ambavyo vimeongeza ushirikiano
na wananchi. Jeshi hilo limeongeza Vikundi 1,778 vya Ulinzi Shirikishi
na kufikia vikundi 6,798 kwa mwaka 2013 kwa Nchi nzima. Vikundi hivyo
vimechangia kupunguza vitendo vya uhalifu Nchini kutoka Asilimia 4.3
mwaka 2012 hadi Asilimia 2.8 mwaka 2013 na hivyo kuchangia kupungua kwa
makosa makubwa na madogo ya jinai kutoka makosa 566,702 mwaka 2012 hadi
makosa 560,451 mwaka 2013.
Mauaji ya Wanawake
9. Mheshimiwa Spika,
pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wananchi
katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, hivi karibuni kumetokea
wimbi la mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake. Katika kipindi cha
Januari hadi Aprili 2014, wanawake wanane (8) wameuawa kikatili katika
Kata za Mugango, Etaro, Nyakatende na Nyegina Wilayani Butiama.
Uchunguzi uliofanyika umebaini kwamba, mauaji hayo yamefanyika mchana na
kwa mtindo unaofanana wa kunyongwa na kanga au kamba na miili yao
kufukiwa kwenye mashimo mafupi au kufichwa vichakani. Mara zote walengwa
ni wanawake wanapokuwa kwenye shughuli zao za kilimo.
10. Mheshimiwa Spika, Serikali
inalaani vitendo hivyo visivyokubalika katika jamii na itawachukulia
hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika kwa namna
yoyote. Serikali imechukua hatua kadhaa za kudhibiti vitendo hivyo vya
mauaji ikiwa ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa 26 na kati yao 13
wamefikishwa mahakamani. Vilevile, Jeshi la Polisi limeunda kikosi kazi
kwa ajili ya kudhibiti hali hiyo na kufanya mikutano ya kuhamasisha
jamii kuhusu kuanzisha na kuimarisha vikundi vya Polisi Jamii. Nitoe
wito kwa wananchi wema, wenye upendo na Nchi yetu kutoa taarifa za
uhalifu na wahalifu kwenye vyombo vya usalama ili Sheria ichukue mkondo
wake.
