Majeneza
yenye miili ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani waliofariki
dunia baada ya kugongwa na basi wakati wakipima ajali katika kijiji cha
Utaho wilani Ikungi mkoa wa Singida kabala ya kuagwa na kusafirishwa
kwenda makwao. Picha na Gasper Andrew
Wakati
miili 15 ya marehemu waliofariki dunia kwa kugongwa na basi katika
Kijiji cha Utaho mkoani Singida ikizikwa juzi, imeelezwa kuwa eneo hilo
limekithiri kwa ajali hadi kuwatisha wanakijiji.
Wakazi
wa kijiji hicho walisema jana kuwa ndani ya miaka minne, zaidi ya watu
50 wamepoteza maisha katika eneo hilo kutokana na ajali kiasi cha
kuingiza hisia za imani za kishirikina.
Mmoja
wa wakazi wa kijiji hicho, Selemani Kinanda alisema: “Kwa miaka minne
iliyopita, ukiacha marehemu 15 wa juzi, watu karibu 50 wamepoteza
maisha. Wengi ni vijana wa kiume.”
Alisema
naye aliwahi kupata mikasa katika eneo hilo na kujikuta amejibamiza
kwenye gari na kuhama barabarani hadi kichakani na baiskeli yake, baada
ya kuona ‘mauzauza’ kwenye eneo hilo.
“Kwanza
yule aliyegongwa kwanza na kusababisha yote haya hatujui alitokea wapi,
pia kulikuwa na sababu gani kwa dereva huyu wa basi kuwafuata watu hao
wote pembeni na kuacha barabara kubwa kulia kwake? Hatukusikia gari ni
bovu wala tairi limepasuka, lazima kuna mkono wa mtu,” alisema Fatuma
Shabani, aliyefiwa na kaka yake.
Hata
hivyo, taarifa kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani zinasema kuwa
hakuna takwimu zozote zinazoonyesha idadi ya ajali au vifo katika eneo
hilo, zaidi ya ile ya juzi yenye takwimu sahihi.
Majonzi kijijini
Kijiji
kizima cha Utaho tangu juzi kilikuwa katika majonzi na simanzi, hata
baada ya miili ya marehemu wanane wa ukoo mmoja na wengine saba
wahamiaji kutoka vitongoji vya Maguha na Kinyaghaa kuzikwa katika
makaburi ya kimila kijijini hapo.
Kutokana na familia nyingi kuwa na msiba, watu walionekana wakitoka nyumba moja kwenda nyingine kutoa pole.
“Msiba
ulikuwa mgumu, tulikuwa tukichimba kaburi hapa tunazika, tunakwenda kwa
mwingine. Kilio hiki ni cha ajabu na miujiza sana kwetu,” alisema
Ramadhani Nyange (74) na kuongeza: “Tunashindwa tuanzie wapi au kwa
nani, maana sisi wote ni ndugu, tumeoleana na kuzaliana kutoka kwa babu
yetu Bulali Masuja ambaye ni mwanzilishi wa kijiji tangu mwaka 1972.”
Alisema kuna haja ya kufanya mkutano wa ukoo ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Watu
hao ni miongoni mwa 19 waliokufa katika ajali hiyo wakiwamo mwenyekiti
wa kijiji, ofisa mtendaji wa kijiji na mwenyekiti wa kitongoji pamoja na
askari polisi wanne. Watu wengine wanane walijeruhiwa.
Aidha,
wananchi hao walionyesha wasiwasi juu ya shughuli za maendeleo baada ya
kufiwa na viongozi wote na juu ya Sh10 milioni za kijiji zilizoko
benki.
Mazishi ya polisi
Mazishi
ya askari F 6837 PC Jumanne Mwakihaba yalifanyika jana saa 7:00 mchana
katika makaburi ya Kisarawe Mjini, yakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya
ya Kisarawe (OCD), Issa Lutavi.
Mwili
wa marehemu ulifikishwa nyumbani kwao Kisarawe alfajiri jana na
ulizikwa kwa taratibu za kijeshi. Mwakihaba alijiunga na jeshi hilo
Agosti 30, 2004 na kupangiwa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani
Singida ambako mauti yamemkuta.
Habari zilizopatikana mkoani Kilimanjaro, zilisema kuwa mwili wa G. 7993 Novatus Tarimo utazikwa kesho huko Tarakea, Rombo.
Kikwete atuma salamu
Rais
Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida,
Dk Perseko Kone kutokana na ajali hiyo iliyosababisha vifo hivyo.
Taarifa
ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema jana kuwa Rais
amesikitishwa na ajali hiyo iliyopoteza nguvu kazi muhimu kwa ujenzi wa
Taifa.
“Vifo
hivi hakika vimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa familia, ndugu, jamaa
na marafiki wa marehemu,” taarifa hiyo ilimkariri Rais Kikwete.
Pamoja
na kuwahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba
huo, Rais Kikwete aliwaombea kwa Mungu watu wote waliojeruhiwa wapate
kurejea haraka katika hali zao za kawaida.
MWANANCHI
