Miongoni mwa habari kubwa wiki hii ni hii ya
bomu kulipuliwa kwenye kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT)
Mwanza ambapo lilijeruhi mtu mmoja alielazwa hospitali ya Bugando.
Mkuu wa dayosisi Askofu Andrew Gulle anasema: "May 5 2014 bomu
limelipuka katika usharika wa kanisa kuu Imani kwenye eneo la rest house
saa mbili usiku, ni bomu la kutengenezwa kwa mkono na lilikua limewekwa
kwenye karatasi za kufungia zawadi na kuwekwa kwenye mfuko wa plastiki
na kuwekwa kwenye varanda ya rest house yetu.
"Kifurushi hicho kimekuwepo kuanzia siku ya Ijumaa ambapo ilipofika
Jumatatu saa mbili usiku muhudumu wa rest house Benadertha alianza
kujiuliza kifurushi hicho kina nini na kwanini kimekuwepo hapo kwa siku
tatu? ambapo mwishowe aliamua kukifungua ili kujua kuna nini ndani
lakini ghafla bomu lililipuka kwa kishindo na moshi mwingi huku
likisambaza misumari midogomidogo na kumjeruhi miguuni na usoni..
"Alikimbizwa hospitali ya rufaa ya Bugando na kufanyiwa upasuaji na
kulazwa kwenye wodi ya mifupa, hatujui lengo la wahusika lilikua
kumuumiza yeye au wengi zaidi, au walishindwa kulifikisha walipotaka
lifike?
"Vikao vya kanisa vimekaa kutafakari na sasa natamka kama kiongozi
wa Dayosisi yale tuliyokubaliana kuyasema kwa Watanzania……
"Tunalaani
kitendo hicho kilichofanyika kwenye eneo la Kanisa, tunaomba makanisa
yetu kuboresha ulinzi katika maeneo yetu yote maana kwa sababu hatuwezi kujua
watu hawa wamekusudia kuweka mabomu wapi na wapi.
"Tunaomba serikali ihakikishe inawashika waliohusika na kutokomeza
mtandao huu wa ugaidi kabla haujaota mizizi na kuhatarisha amani
tuliyoizoea Tanzania.
"Mwisho tunatoa wito kwa Wakristo wote wawe watulivu, wasiogope wala
wasitishwe na mashambulizi yanayotendeka, tunatoa wito kwa Wakristo wote
kwamba kusitokee fujo popote wala kulipiza kisasi, silaha yetu kubwa ni
maombi na kumtegemea Mungu, wakati huu kanisa linapoteswa ndio wakati
wa kumtegemea Mungu zaidi na kuhubiri habari njema"
