DAR ES SALAAM Aprili 27, 2014 … Wakazi wa kusini mwa
Tanzania yaani mkoa wa Mtwara wametakiwa kukaa mkao wa kula burudani ya
nguvu ya muziki itapigwa moja kwa moja jukwaani siku ya tarehe 2 ya
mwezi wa Mei katika ukumbi wa Makonde Club.
Mwanamuziki Diamond atafanya shoo laivu mkoani Mtwara chini ya
udhamini mkubwa wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania
akisindikizwa na kipenzi chake, Malkia wa Bongo Movie nchini, Wema
Sepetu – ‘Beautiful Onyinye’ au Madame kama mashabiki wake wanavyopenda
kumwita.
Msanii Diamond ambaye kwa sasa ndiyo mwenye mafanikio makubwa ya
kimuziki nchini amekuwa ni kivutio kikubwa kwa mashabiki wa ndani na nje
ya nchi kila mahali anapoalikwa kufanya shoo na hivyo kujizolea sifa
lukuki na hata kuchaguliwa kuwania tuzo mbalimbali za muziki barani
Afrika.
Akizungumzia juu ya shoo hiyo ya kukata na shoka kwa wakazi wa mkoa
wa Mtwara, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,
Kelvin Twissa amebainisha kuwa tukio hili limeandaliwa ikiwa ni sehemu
ya burudani kwa wateja wetu, kufurahi kwa pamoja na kuwashukuru wateja
wetu kwa kuendelea kutumia huduma zetu.
“Hakuna kitu ambacho tunajali na kukithamini kama wateja wetu,
haijalishi wawe kona gani ya Tanzania, walipo popote tutawafikia.
Vodacom imekuwepo nchini kwa zaidi ya miaka kumi sasa na kwa kipindi
chote hicho watanzania wameonyesha kutuunga mkono na kutufanya tuwe
mtandao unaaongoza kwa mawasiliano nchini.” Alisema Twissa.
Kwa kuongezea Twissa amewataka wakazi na mashabiki wote wa Diamond na
muziki wa Bongo Flava kujitokeza kwa wingi kwani mbali na burudani
kutakuwepo na huduma na bidhaa mbali mbali za Vodacom.
Katika kunogesha shoo hiyo kwa wakazi wa kusini Malkia wa Bongo Movie
nchini, Wema Sepetu naye akasema haitokuwa poa kama asipomsindikiza
asali wake wa moyo kwenda kujivinjari pande hizo na mashabiki wao. Kwa
tafsiri nyingine mashabiki wa Mtwara wanabahati kubwa ya kutembelewa na
mastaa wawili wakubwa kutoka tasnia mbili tofauti nchini.
“Hii shoo si ya kukosa kabisa kwani hakuna kiingilio bali ni uwepo
wako tu na kujiandaa kwako kwa burudani ndio kinachohitajika.
Tunawapenda sana wateja wetu wa Mtwara, hatuna uwezo wa kulipa kutokana
na kuwa wateja wetu waaminifu siku zote lakini ninaamini kwa pamoja
tunaweza kujumuika na kufurahia wakati tulionao. Naombeni mjitokeze kwa
wingi, rafiki amlete rafiki yake ili tuwe pamoja siku hiyo.” Alimalizia
Twissa.
