Watu wawili wamefariki dunia papo
hapo na wengine kumi na mmoja kujeruhiwa vibaya wakati wakifanya kibarua
cha kushusha nguzo za kusambazia nishati ya umeme vijijini kupitia
kampuni ya moja ya Derm katika kijijini cha Bisumwa wilayani Butiama
mkoani Mara.
Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo wamesema tukio hilo limeokea leo saa
3.30 asubuhi katika kijiji cha Bisumwa wilayani Butiama,ambapo vibarua
hao kutoka kijiji cha sabasaba baada ya kufika kijijini hapo na lori
hilo aina ya Scania yenye namba za usajili T 787 CUL wakiwa juu ya
sheena hiyo ya nguzo na wakati wajaribu kufungua mikanda kwa ajili ya
kuzishusha nguzo hizo zilishuka kwa kasi kubwa sambamba na wao hatua
ambayo imesababisha watu wawili kufariki dunia kwa kugongwa na nguzo
hizo huku wengine wakipata majeraha makubwa yakiwemo ya kuvunjika kwa
miguu.
Viongozi wa halmashauri ya Butiama
wakiongozwa na mwenyekiti wake Bw Magina Magesa, ambao walifika muda
mfupi baada ya tukio hilo kutokea kwa ajili ya kutoa msaada kwa majeruhi
hao,pamoja na kutoa pole lakini wametaka kampuni zinazohusika
kusambaza nishati ya umeme katika vijiji vya mkoa wa Mara kuchukua
tahadhari wakati wa kusafirisha nguzo hizo ili kuepuka ajali mbaya kama
hiyo.
Kaimu kamanda wa polisi wa polisi
mkoa wa Mara kamishina msaidizi wa jeshi la polisi Paul Kasabago,
akizungumza kwa njia ya simu amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo
na kuwataja marehemu kuwa ni Masui Magibo (20) na Salabanze John (22)
wote wakazi wa kijiji cha Sabasaba wilayani Butiama na kwamba majeruhi
wote wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Mara mjini Musoma kwa ajili
ya matibabu zaidi.