VYETI VYA KUZALIWA SASA KUTOLEWA MASHULENI



Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mfaranyaki, Ruvuma wakifurahia jambo.
 
*************

Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) ameanzisha mpango wa uandikishaji na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wanaoanzia umri wa miaka sita hadi 18 katika shule zote za msingi na sekondari nchini.

Hatua hiyo inatokana na kubaini kuwa ni asilimia 23 tu ya Watanzania nchini ndio waliosajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango huo kwa Manispaa ya Ilala  Dar es Salaam jana, Meya wa Manispaa hiyo, Jerry Silaa, alisema   utasaidia kuongeza idadi ya Watanzania wenye vyeti vya kuzaliwa ambavyo ni tiketi ya kupata mahitaji muhimu na kutambulika kama wazawa wa nchi.
 

“Asilimia 23 ni ndogo sana, hasa ikizingatiwa kuwa vyeti vya kuzaliwa ni nyaraka muhimu kwa raia yeyote, ili apate mahitaji muhimu nchini mwake kama vile hati ya kusafiria, kusoma, kitambulisho cha uraia na hata haki ya kupiga kura,” alisema Silaa.

Alisema mpango huo ambao unaanzia Ilala utaanza na shule za msingi za Serikali ambapo watoto wasiokuwa na vyeti hivyo, kupitia walimu waliopewa mafunzo maalumu ya usajili na utoaji vyeti hivyo, watasajiliwa na kuvipata ndani ya wiki moja.

Hata hivyo, alionya walimu waliochaguliwa kushughulikia usajili huo, kuhakikisha kuwa wanatanguliza uzalendo na kusajili na kutoa vyeti kwa watoto ambao wamehakikiwa na kuthibitika kuwa ni Watanzania na si vinginevyo.
 

“Napenda kueleza, kwamba kumekuwa na changamoto ya kukosa uaminifu kwa watendaji wengi wa Serikali, ambao wanaaminiwa kukusanya fedha. Nasisitiza kwamba fedha ya Serikali ni lazima iwasilishwe inakotakiwa kwa njia sahihi.
 

“Naamini walimu mtakuwa waaminifu na atayefanya kinyume, sheria itachukua mkondo wake. Naamini walimu wa Manispaa yangu hamtaniangusha katika hili,” alisisitiza.
 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Rita, Philipo Saliboko, alisema katika kutekeleza mpango huo, Wakala huyo ameamua kushirikisha walimu na waratibu katika usajili na uhakiki wa watoto hao ambapo hatua ya mwisho itafanywa na watendaji wa Rita kwa kuhakiki taarifa za watoto hao na kutoa vyeti.

“Awamu ya kwanza ya mpango huu, tumeamua kuanzia Dar es Salaam, katika manispaa ya Ilala, na itafutiwa na Kinondoni na kumalizikia Temeke. Katika mikoa mingine bado mchakato wa kifedha unaendelea ili kuendelea na mpango huu,” alisema Saliboko.

Alisema Ilala jumla ya walimu 105 na waratibu 28 ndio watashiriki  kusajili watoto hao kwa kuzungumza na wazazi wao na kuhakiki taarifa zao kabla ya kuziwasilisha Rita kwa uhakiki zaidi na kuchapishwa kwa vyeti hivyo.

Akizungumzia shule za msingi na sekondari binafsi, Saliboko alisema watatumia walimu waliopewa mafunzo, lakini pia watashirikisha taasisi muhimu kama Uhamiaji ili kutotoa vyeti kwa watoto wasio wazawa wa Tanzania


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo