SHEIKH WA MSIKITI MKUU WA BONDENI ARUSHA AMWAGIWA TINDIKALI



Sheikh wa Msikiti Mkuu wa Bondeni mkoani Arusha, Mustaph Kiago (49) na mwanaye Khalid Mustapha (10), wamemwagiwa kimiminika kinachodhaniwa kuwa ni tindikali wakati wakiingia msikitini.

Sheikh  Kiago amejeruhiwa shingoni na mtoto wake ameumizwa machoni na wote wanatibiwa hospitali ya mkoa ya ya Mount Meru .

Akizungumza nasi nje ya wodi ya watoto kwenye hospitali hiyo jana, Kiago alisema amemwagiwa tindikali hiyo jana saa 11.10 alfajiri wakati anashuka ngazi kuingia msikitini kuongoza sala ya alfajiri.

“Nilipomaliza ngazi ili niiingie msikitini nilimwona kijana nyuma yangu ameshika kopo lenye maji mekundu na ghafla alinimwagia usoni na mengine yalimpata mtoto wangu”, alisema.

Alisema mtuhumiwa huyo alikimbia baada ya kuwajeruhi akitumia pikipiki iliyokuwa nje ya msikiti.

Aliendelea kusema kuwa baada ya mtu huyo kukimbia, alirudi ndani na kumchukua mtoto wake hadi hospitali ya Mkoa Maunt Meru na kugundua kuwa ameumia macho wakati yeye alichunika ngozi ya shingo na usoni.

Mustapha aliyekuja nchini hivi karibuni akitokea Misri, alisema ameumia macho na kwamba ana wasiwasi jicho la kushoto halitaona tena.

Sheikh huyo alisema chanzo cha tukio hilo ni vita iliyoanza muda mrefu ambapo, Februari 7 mwaka huu, akiwa msikitini, alifuatwa na Sheikh wa Mwanza (jina linahifadhiwa), akiwa na watu kadhaa na kutakiwa kutangaza jihad misikiti yote ya Arusha.

Alifafanua kuwa alikataa kutangaza jihad ambayo ni vita ya silaha dhidi ya Waislamu na wasio Waislamu akisema;“Nilipinga kwa sababu hatuwezi kuvunja amani tulionayo kwa masuala ya dini, wakaniambia lazima wataniua,"alisema.

Alifafanua kuwa alipowapinga ikatokea vurugu kubwa pale msikitini ambapo miongoni mwa kundi hilo lililoongozwa na Sheikh wa Mwanza aliyemtaja (jina tunalo),  alimrukia na kumpokonya kipaza sauti lakini naye akakimbilia kuzima umeme.

Alisema waumini waliokuwepo walituliza ghasia naye alikwenda kutoa taarifa polisi.

Alilalamika kuwa licha ya kufika asubuhi hospitalini mtoto wake hajapata kitanda hivyo alikuwa anamshughulikia kwanza mwanae.

Mtoto Khalid anayesoma darasa la tatu nchini Misri, hakuzungumza kwa kuwa hafahamu Kiswahili na anazungumza Kiarabu.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Japhet Lusingu, akizungumzia tukio hilo, alisema polisi ina taarifa zake na inaendelea na uchunguzi.

Alisema mara baada ya tukio hilo, polisi ilijulishwa na kufika eneo la tukio na kufanya mahojiano na mashuhuda kisha kuchukua kopo linalosadikiwa kuwa lilikuwa na tindikali hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo