Hivi
karibuni Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) ulizindua zoezi
la Usajili na Kutoa vyeti katika Shule za Msingi katika Manispaa ya
Ilala Jijini Dar es Salaam. Zoezi hili ni sehemu ya utekelezazji wa
Mkakati wa Usajili wa Watoto walio na Umri kati ya Miaka 6-18 ( 6-18
Birth Registration Initiative) uliobuniwa ili kukabiliana na changamoto
ya wananchi wengi kutosajiliwa na kuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Katika
zoezi hili, RITA inashirikiana na Manispaa ya Ilala kupitia Idara ya
Elimu. Kila shule imeteua mwalimu mmoja anayeratibu Usajili katika shule
husika na Wanafunzi wasio na vyeti wamapewa fomu za maombi
zitakazojazwa na wazazi wao na baada ya hapo hurejeshwa RITA kwa ajili
ya uhakiki na kuandaa vyeti. Baada ya vyeti kukamilika, vitapelekwa kwa
Mwalimu Mratibu ambaye atavigawa kwa wanafunzi husika.
Katika
wiki mbili za kwanza za utekelezaji, mwamko umekuwa mkubwa sana kwani
Jumla ya wazazi 16,500 wameshachukua fomu kwa ajili ya kuomba kupata
vyeti vya kuzaliwa vya watoto wao na mpaka sasa zaidi ya fomu 1649
zimeshajazwa na kurejeshwa RITA ambazo ni kutoka shule 35 . Jumla ya
shule za Msingi 105 zinashiriki katika zoezi hili zenye jumla ya
wanafunzi 139,808.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka shule mbalimbali, wazazi na walezi wengi
wameonyesha kufurahia zoezi hili kwani huduma zimesogezwa katika maeneo
yao pamoja na utaratibu mzima unaotumiwa katika kuhakikisha kila mtoto
anapata cheti cha kuzaliwa. Vyeti vinavyotolewa kwa watoto ni vya
kawaida kama vinavyotolewa katika ofisi zozote za RITA na taratibu zote
za uhakiki hufanyika kabla ya mwanafunzi kupewa cheti.
Kwa
mujibu wa Takwimu, ni wananchi asilimia 23 tu wamesajiliwa na kupata
vyeti nchini ikiwa ni idadi ndogo sana kulinganisha na umuhimu wa Vyeti
vya kuzaliwa kwa kila mwananchi. Tunaamini kwamba mkakati huu utakuwa
sehemu ya suluhisho ya changamoto hii na unatamewa kuenezwa katika
Wilaya nyingine za Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia Mwezi Juni mwaka huu.
Vile vile utaratibu unaandaliwa ili kuweza kuzihushisha shule za
Sekondari
Tunawahamasisha
wazazi wajitokeze kuwasajili watoto katika shule za msingi wanazosoma
ili kuwapata vyeti vya kuzaliwa. Hakuna sababu ya mwanafunzi yoyote
kutokuwa na cheti cha kuzaliwa katika eneo zoezi hili linatekelezwa
kwani huduma imesogezwa karibu na maeneo wanayoishi. Ikumbukwe kwamba
watoto wanaopata vyeti sasa watakuja kuvitumia kujiunga na elimu ya
sekondari, kupata nafasi ya kusoma katika Vyuo Vikuu, kupata mikopo ya
Masomo elimu ya juu, kupata kazi, kupata kitambulisho cha Taifa
wakifikisha miaka 18, kufungua akaunti, kupata pasi ya kusafiria na
matumizi mengine.
Phillip Saliboko
Afisa Mtendaji Mkuu – RITA