Serikali
imesema itaendelea kuboresha Sekta ya elimu nchini ili kuongeza
wataalamu watakaosaidia kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za mitaa Mh. Hawa Ghasia wakati wa mkutano na waandishi wa
habari leo jijini Dar es salaam.
Waziri
Ghasia alisema kuwa baada ya Serikali kwa kushirikiana na wananchi
katika maeneo mbalimbali hapa nchini kukamilisha ujenzi wa shule za kata
hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa shule hizo zinakuwa na vitabu,
maabara za kisasa pamoja na walimu wakutosha.
Akifafanua
zaidi alisema shule kongwe za Sekondari nchini ni miongoni mwa shule
zitakazoboreshwa ili kutoa wanafunzi wenye ubora na uwezo ili kulisaidia
taifa katika siku za usoni kuwa na wataalamu wakutosha katika maeneo
yote yatakayosaidia kuwaletea wananchi maendeleo.
Pia
Waziri Ghasia alieleza kuwa maboresho hayo yanakwenda sambamba na
kuongeza idadi ya vyuo vya Elimu ya kati na vile vya Elimu ya juu .
Katika
kutekeleza mpango wa kuboresha elimu Waziri Ghasia amesema kila
Mtendaji katika Mkoa na halmashauri zote nchini anatakiwa kusimamia
vyema utekelezaji wa mpango huo ili kuinua kiwango cha elimu na wale
watakaoshindwa Serikali itawachukulia hatua kali za kinidhamu.
Katika
Hatua nyingine Waziri Ghasia amesema Serikali itahakikisha kuwa mfumo
mpya wa ukusanyaji mapato katika Halmashauri zote nchini unafungwa
kufikia mwaka 2015/16 ili kusaidia kuongeza mapato na kuboresha huduma
za jamii kama hosipitali, Elimu na maji.
Alitaja
Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kuwa miongoni mwa halmashauri
zilizokwisha anza kutumia mfumo wa kielektroniki katika kukusanya mapato
yake ambapo mfumo huo unaainisha vyanzo vyote vya mapato katika eneo
husika hivyo kurahisisha ukusanyaji wa mapatao hayo.
Akifafanua
zaidi alibainisha kuwa kufuatia maboresho yanayoendelea Kufanywa na
Serikali hati safi katika Halmashauri zimeongezeka kutoka halmashauri 53
za mwaka 2005/2006 hadi Halmashauri 104 za mwaka 2011/12.
Pia
Serikali Imeendelea kuchukua hatua za kinidhamu na Kisheria kwa
watumishi wachache waliobainika kujihusisha na ufujaji wa mali za umma
ambapo hadi Septemba, 2013 jumla ya wakurugenzi 53, Wakuu wa Idara 65 na
watumishi 749 walichukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa
kuhusishwa na ubadhirifu wa fedha za umma.
