Dodoma, Tanzania. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe Leo amehojiwa na Kamati ndogo ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi CCM), akiwa ni mmoja wa vigogo waliokuwa wakituhumiwa kuanza kipita huku na kule kwa ajili ya kuonyesha nia ya kugombea urais mwaka 2015.
Membe ameieleza kamati kwamba CCM inatakiwa kumtangaza mgombe urais kabla ya Disemba, mwaka huu.
“Nafikiri wakati umefika sasa kwa CCM kuchagua mgombea urais mapema, au kuwachagua viongozi wanaofaa kugombea nafasi hiyo ili mdahalo ufanyike, wananchi wamjue mgombea urais mapema,” amesema Membe.
Ndani ya kamati hiyo Membe amesema hivi punde kwamba alihojiwa maswali magumu kuhusu urais pamoja na mambo mengine. Lakini akaenda mbali na kusema kuwa si yeye tu bali hata wengine waliohojiwa nao waliulizwa maswali magumu.
“Kamati inauliza maswali mazito na magumu yanayohusiana na uvunjaji wa maadili ya uongozi wa chama chetu. Kamati ya maadili imejipanga vizuri wala msidanganyike,” amesema Membe
Membe amesema moja ya swali kubwa wanaloulizwa ni kuzuka kwa makundi makubwa mara anapojitokeza kiongozi na kuonyesha nia ya kugombea urais.
Kamati ndogo ya Maadili ya CCM, inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Cham hicho Bara, Philip Mangula na anahoji kuhusu mikakati ya vigogo hao kuelekea uchaguzi wa 2015.