Bw Simon Ndiani ambaye ni babake Isaack Ndiani akiongea na wanahabari
nje ya shule ya St Charles Mutego Februari 11, 2014. Picha/ANN KAMONI
Na OUMA WANZALA
POLISI wamekubali kuwa mwanafunzi aliyekufa katika shule ya St Charles Mutego Education Centre, Lenana, Nairobi, mnamo Jumapili usiku alipigwa risasi kimakosa na mmoja wao.
OCPD wa Dagoreti Mathew Gwiyo alidai kuwa marehemu aliuawa na polisi waliowafyatulia risasi wavamizi ambao walikuwa wakitoroka.
“Tunachunguza
jinsi alivyoweza kuwa miongoni mwa wavamizi hao ndipo akapigwa risasi.
Polisi hawakuweza kutambua kuwa alikuwa mwanafunzi kwa sababu hakuwa
amevaa sare rasmi za shule bali alikuwa amevaa suruali aina ya jeans,”
akasema Bw Gwiyo.
Bw Gwiyo
aliongeza kuwa mwanafunzi huyo, ambaye alitambiliwa kama Isaac Lesile,
mwenye umri wa miaka 20, alikufa kilomita moja kutoka shuleni.
Mwili wake
ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City, Nairobi. Hapo
jana, baba yake, Bw Simon Ndiami, alitaka uchunguzi wa kina ufanywe
kuhusu kisa hicho alichotaja kuwa cha kusikitisha.
“Sielewi ni
kwa nini polisi walimuua mwanangu ambaye alikuwa akiwatoroka wavamizi,”
akasema Bw Ndiami. Mwanafunzi huyo wa Kidato cha Kwanza alikuwa
amejiunga na shule shule hiyo Jumatano wiki jana. Bw Ndiami alidai kuwa
wanafunzi wa shule hiyo walikuwa wamepigana mchana na shambulizi hilo la
usiku lilitokana na mzozo huo.
“Ni jambo la
kusikitisha sana kwamba mvulana huyo aliuawa na polisi ambao
walitazamiwa kumuokoa kutoka kwa shambulizi hilo. Alipigwa risasi
kichwani kutoka upande wa nyuma, ishara tosha kwamba alikuwa akitoroka,”
akasema mzazi huyo. Mnamo Jumapili watu waliojihami walishambulia shule
hiyo mwendo wa saa tano usiku na kuwajeruhi wanafunzi zaidi ya 40.
Washambuliaji waliingia shuleni baada ya kuvunja ua uliojengwa kwa mbao
na kwenda moja kwa moja hadi kwenye mabweni ambako waliwaagiza wanafunzi
wote watoke nje.
“Washambuliaji
hao ambao walikuwa wamejihami kwa silaha butu walisimama kwenye lango
kuu la bweni na kuamuru ufunguliwe kabla ya kutuagiza tutoke nje.
Walitumia mbao na mapanga kutupiga mmoja baada ya mwingine,” wanafunzi
wakasimulia.
Nyimbo za kivita
Walisema kuwa
wakati huo washambuliaji waliimba nyimbo za kivita za jamii ya
Wamasaai. Wanafunzi pia walisema washambuliaji hao ambao walikuwa
wamefunika nyuso zao, waliwapiga bila huruma ambapo baadhi ya wasichana
walizimia.
Mnamo
Jumatatu, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw Bonface Makori ,alidai kuwa
baadhi ya wanafunzi waliwasaidia washambuliaji kuingia shuleni.
“Tuko na
habari kwamba baadhi ya wanafunzi walijiunga na washambuliaji na hata
kuwasaidia kutoroka,” akasema Bw Makori. Aliwakashifu baadhi ya wazazi
aliosema hukataa kutoa habari zaidi kuhusu watoto wao wanapotaka
wasajiliwe shuleni humo.
