Madiwani wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Manispaa ya Shinyanga wametanganza kujiuzulu nyadhifa zao wakidai uongozi ngazi ya taifa wa chama hicho unaendekeza majungu na kudhalilisha baadhi ya viongozi kwa kuwaita wahaini au wasaliti bila kuchambua ukweli.
Madiwani hao, Sebastiani Peter kutoka kata ya Ngokolo na Zacharia Mfuko
kutoka kata ya Masekelo, jana walizungumza na waandishi wa habari mjini
Shinyanga na kusema wamechukua uamuzi huo kutokana na makosa
yaliyofanywa na viongozi wa kitaifa wa Chadema kwa nyakati tofauti.
Peter alitaja sababu tatu zilizopelekea kujiuzulu kwake, ya kwanza
alisema ni Novemba mwaka 2013 kikundi cha ulinzi cha chama hicho (Red
Brigade) kiliandika barua kwa Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa kuwa wamehongwa Sh. milioni 90 na CCM kukisaliti chama
chao.
Alisema sababu ya pili ni kutokana na kutotimizwa kwa ahadi ya
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ya kujenga nyumba ya aliyekuwa
mgombea ubunge wa chama hicho Jimbo la Shinyanga Mjini, marehemu
Shelembi.
Jambo la tatu alisema ni tabia iliyozuka ndani ya chama hicho
kuwadhalilisha viongozi wa chini kwa kuwabatiza majina mbalimbali kama
wasaliti na wahaini wa chama.
Kwa upande wake, Masekelo alisema uamuzi wake wa kujiuzulu ni kutokana
na kuwapo ubabaishaji ndani ya chama hicho na kwamba kuna sakata la
mwenyekiti wa mtaa kukigawa kiwanja huku kukiwa na kamati ya ugawaji
lakini aliwaeleza viongozi wa chama mpaka sasa hakuna kinachoendelea.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Manispaa ya Halmashauri ya Shinyanga
ilipata madiwani 18, kati yao 10 ni wa CCM na wanane Chadema.
