Imebainika kuwa dawa za Serikali zikiwamo za kurefusha maisha
kwa waathirika wa Ukimwi zinauzwa katika maduka ya dawa baridi na maduka
bubu ya watu binafsi katika Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Uchunguzi wa
gazeti hili umebaini kuwa maduka yanayouza dawa hizo mengi yanamilikiwa
na watumishi katika vituo vya afya vya Serikali, wakati dawa zinazouzwa
ni zile ambazo hutolewa na Serikali kwa ajili ya kupelekwa kwenye
Zahanati na Vituo vya Afya kwa ajili ya wagonjwa.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa afya za wanunuzi na
watumiaji wa dawa katika maduka husika ziko hatarini kutokana na
mazingira yasiyoridhisha ya maduka husika, huku wahudumu au wauzaji
katika maduka hayo wakibainika kuwa kuwa si watu wenye elimu ya
ufamasia.
Katika Kijiji cha Changuge kata ya Mirare,
ilibainika kuwa dawa zikiwamo ARV zinapatikana kwa urahisi katika duka
linalomilikiwa na mtumishi anayefahamika kwa jina la Nicolaus Joseph,
ambaye ni Muuguzi wa Kituo cha Afya cha Serikali, Changuge.
Uchunguzi huo pia ulibaini kwamba dawa hizo pia
zinauzwa katika duka la mtumishi mwingine wa kituo hicho, Pamela Otuma
ambalo liko katika Kijiji cha Nyambogo, Kata ya Kitembe Wilayani Rorya.
Hata hivyo, Joseph na Otuma kwa nyakati tofauti
walikanusha kuuza dawa za ARV pamoja na nyingine, licha ya kila mmoja
wao kukiri kwamba aliwahi kumiliki duka la dawa siku zilizopita.
Joseph alisema duka la dawa alilikuwa akilimiliki
lilifungwa Februari mwaka jana baada ya kubainika kwamba kufunguliwa
kwake hakukufuata taratibu za kifamasia.
“Nilikuwa na duka ambalo lilikuwa likiniingizia
kipato cha ziada, lakini sikuwahi kuuza dawa za Serikali, hata hizo
tuhuma zilipotolewa ukaguzi ulifanyika na sikukutwa na dawa zozote
kwenye duka,” alisema Joseph na kuongeza:
“Baada ya kufungiwa niliuzwa dawa zilizokuwepo kwa
watu wengine wenye maduka na hivi sasa najiandaa kufuata taratibu za
kifamasia ili niweze kufungua tena duka langu”. Kwa upande wake Otuma
alisema : “Mimi sijawahi kuuza dawa za Serikali katika duka langu, na
duka hilo lilikuwa Kijiji cha Nyambogo lakini kulipoanza kuwepo maneno
kwamba nauza dawa za Serikali nikalifunga”.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Rorya, Ephraem Ole Nguyaine alisema malalamiko ya kuuzwa kwa dawa hizo
nje ya taratibu yamefika ofisini kwake na kwamba ilikuwa sababu ya
kuhamishwa kwa watumishi wa afya akiwamo aliyekuwa Mganga Mkuu wa wa
Wilaya hiyo, Daniel Chacha.
“Ninashangaa dawa hizo kudaiwa kuwa bado
zinaendelea kuuzwa katika maduka ya mitaani, kwa kweli nitafuatilia
zaidi suala hili,” alisema Ole Nguyaine.
Wanaoshi na VVU
Baadhi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi
walikiri kununua ARV na dawa nyingine katika maduka hayo ya watu binafsi
kutokana na kile walichokieleza kuwa ni uhaba wa dawa hizo katika vituo
vya Serikali.
CHANZO: MWANANCHI
“Nikweli ARV zinauzwa hapa senta ya Changuge kwenye duka la
mtumishi wa Kituo cha Afya Changuge watu wananunua pindi dawa hizo
zinapokosekana kituo cha afya na dawa hizo gharama yake kwa kopo moja ni
kuanzia Sh5, 000,” anasema mmoja wa wagonjwa ambaye aliomba jina lake
lihifadhiwe kwa kuofia kwamba huenda akanyanyapaliwa.
Dawa hizo pia zinauzwa katika Mji Mdogo wa
Shirati. Mkazi wa Kijiji cha Kyariko, Monika Onyango alisema: “…Ni kweli
dawa za ARV wakati mwingine zinapokosekana hospitalini tunazinunua
kwenye maduka ya dawa baridi kwa Sh5, 000 kwa kopo moja la vidonge 60”.
Onyango ambaye ni mtumiaji wa dawa hizo aliongeza:
“Siwezi kumtaja anayeuza kwa jina au kutaja duka kwa sababu
linatusaidia dawa zikikosekana tunazipata huko kwenye maduka binafsi
tunaendelea na dozi”
Alisema wao hawajali hata kama wanauziwa dawa hizo
na nani, kwani wanachokitaka ni kuhakikisha kwamba afya zao
zinaimarika. “Sasa kama dawa zinakosekana hospitali tufanyeje? Inabidi
wagonjwa tukatafute kwenye maduka ya dawa kwa pesa zetu...Hizo ndizo
changamoto tunazokutana nazo sisi tunaoishi na VVU,” alisema.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa uuzwaji wa
ARV katika maduka ya dawa baridi, unachochewa na sababu mbili kubwa;
kwanza ni baadhi ya wagonjwa kukwepa kwenda vituo vya afya, ambako
hulazimika kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu wakisubiri kupatiwa dawa
hizo.
Sababu nyingine ni uhaba wa dawa hizo katika vituo
vya afya, hali ambayo kuwalazimisha wagonjwa kwenda katika vituo hivyo
mara nyingi kuzifuata, hivyo kuchoka kutokana na baadhi yao kutokuwa na
afya nzuri.
Mkazi wa Kijiji cha Changuge, Joice Odello
alisema: “Maduka ya dawa baridi yana wateja wa ARV maana mtu akifika tu
unahudumiwa mara moja, unatoa pesa unapewa dawa unaondoka zako, lakini
ukienda kituo cha afya unatumia muda mwingi kungoja dawa kuna mizunguko
mingi wengine ni watu wenye hishima zao hawawezi kupanga foleni na
wanaona aibu kujulikana ni wagonjwa.”
Onyango kwa upande wake alisema ukosefu wa ARV ni
kero kwao, kwani wakati mwingine zinaweza kupita wiki mbili bila kupata
dawa hizo na wakati mwingine hupewa nusu dozi.
Mbali na uhaba wa ARV, pia kumekuwapo na uhaba wa
dawa nyingine za magonjwa nyemelezi, hivyo wagonjwa wa VVU wamekuwa
wakielekezwa kwenda kununua dawa hizo kwenye maduka binafsi.
Kadhalika agonjwa husika wamekuwa wakilazimika
kubeba gharama za vipimo kama vile x-ray ambayo hutozwa Sh15,000 na
video Sh30,000.
Mkazi wa Rorya, Adelina Joseph alisema:
“Ukimpeleka mgonjwa wa TB gharama ni hizo hizo, ukilazwa unajikuta
unalipishwa hata zaidi ya Sh200,000 pamoja na dawa gharama hizo kubwa
mgonjwa anakufa, tunaomba wagonjwa wa VVU gharama ziwe chini la sivyo
tutazidi kufa”.
CHANZO: MWANANCHI
