MKUTANO Mkuu wa Kijiji cha Olgilai wilayani Arumeru umeazimia kuwachapa viboko vijana wa kiume wanaovaa suruali chini ya makalio pamoja na wanawake wanaovaa sketi fupi na suruali zinazobana. Azimio hilo pia limeelekezwa kwa wanafunzi wanaopata mimba au kuozeshwa na kuacha masomo bila sababu za msingi.
Mkutano huo umepitisha maazimio saba yanayolenga kurejesha nidhamu
na heshima kijijini Olgilai limefikiwa kutokana na vijana wa kike na
kiume kuvaa nguo zisizo na heshima.
Mwenyekiti wa Kijiji cha
Olgilai, Godson Boazi katika barua yake ya Januari 24 mwaka huu kwa
viongozi wa makanisa kijijini hapo, aliwaomba kuunga mkono hatua hiyo
katika kurekebisha tabia ndani ya jamii yao.
“Viongozi wa dini
tunafahamu kazi kubwa ya kutunza kundi la Mungu likae kwenye maadili
mema. Hivyo basi tunaomba mtusaidie jukumu hili ambalo tumeambatanisha
barua kwenu,”alisema Boaz na kuongeza:
“Viongozi wa dini
tumewaandikia waraka huu tukijua kwamba ninyi ni watu muhimu katika
kusaidia jambo hili na kuwafikishia taarifa waumini wenu wote wakubwa
kwa wadogo.”
Katika barua yake ambayo MTANZANIA inayo nakala yake
Mwenyekiti huyo alisema kwa kauli moja uongozi mkutano huo uliafiki
suala hili na kuamuru lianze kutumiwa Januari 24 mwaka huu.
Aliyataja
maazimio yaliyopitishwa kuwa ni vijana wanaokaa au kusimama ovyo
barabarani na maeneo mengine bila shughuli maalumu watachapwa viboko.
Jingine
ni kuwachapa viboko wote watakaovaa nguo zisizofaa katika jamii yao
mfano sketi fupi, suruali zilizobana kwa wasichana na akina mama.
“Vijana
wa kiume wanaovaa suruali zinazojulikana kama mlegezo, uendeshaji ovyo
wa pikipiki, wavutaji wa bangi, dawa za kulevya, gongo na wanywaji wa
viroba, uchezaji kamari na karata.
“Wanaotukana ovyo barabarani
na kupiga kelele za uvunjaji wa amani, wezi wa vitu vikubwa na vidogo
kama kuku, ndizi, viazi, mahindi na mboga shambani watashughulikiwa,”
alisema Boazi.
Alisema Mkutano Mkuu wa Kijiji ulijiridhisha kuwa
matendo hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa nidhamu kijijini
hapo na maeneo mengine.
>>>>>MTANZANIA