SIKU
moja baada ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutoa tamko la kumtaka
aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuacha kukigawa chama kwa madai
kuwa hana sifa kuwa rais, mambo mazito yamezidi kuibuka huku ikitolewa
orodha ya wanachama wa CCM wakiwemo mawaziri, wabunge na makada maarufu
wanaodaiwa kukisaliti chama hicho.
Hatua
hiyo imeenda sambamba na kumtaka Katibu wa Umoja wa Vijana Uhamasishaji
na Chipukizi, Paul Makonda, kuacha kuwanyooshea vidole wenzao, wakati
ndani ya chama hicho kuna wasaliti wakubwa na wasiokuwa na usafi wowote
wa kuwasema wenzao.
Hayo
yamewekwa hadharani Dar es Salaam jana na aliyekuwa Mwenyekiti na
mwanzilishi wa CCJ Taifa, Richard Kiyabo, wakati akizungumza na
waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano Idara ya Habari (MAELEZO).
Kiyabo
aliitaka CCM kusafisha wanachama wasio waaminifu ambao ni mamluki
wakiwemo mawaziri, wabunge machachari na makada maarufu kutokana na
kushiriki kwao kuanzisha Chama Cha Kijamii (CCJ) huku bado hawajarejesha
kadi za chama hicho.
Kiyabo
alisambaza kwa waandishi wa habari orodha ya wanachama wa CCM 37
anaodai walishiriki kutoa michango ya fedha kwa ajili ya kufanikisha
maandamano ya amani ya CCJ yaliyolenga kupinga uonevu wa msajili wa
vyama vya siasa nchini.
Alisema
tayari ameshamwandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip
Mangula kukiomba chama kichukue hatua za kinidhamu na kimaadili kwa
wanachama ambao si waaminifu na tayari walikwishapoteza sifa za kuwa
wanachama, kutokana na kushirikiana nao kuanzisha CCJ, huku wakiwa
wanachama wa CCM.
"Kitendo
cha kuwa wanachama wa vyama viwili kwa wakati mmoja ni kosa kubwa na ni
usaliti ndani ya chama, kosa hili halipishani na kosa la uhaini ndani
ya chama, lakini kwa masikitiko yangu makubwa watu hawa hadi sasa
hawajaitwa na vikao vya chama wala hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa au
kujadiliwa kwa makosa ya kukisaliti chama na kuamua kuwa mamluki ndani
ya chama," alisema Kiyabo.
Alisema
mwanzoni mwa mwaka 2010 walipokubaliana kuanzisha CCJ malengo makuu
ilikuwa chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu na kusimamisha mgombea wa
kiti cha urais na wabunge, pamoja na madiwani kama wangekidhi matakwa ya
kisheria.
"Nashangaa
ndani ya CCM bado kuna wanachama na viongozi waandamizi wana kadi mbili
za CCJ na CCM na wanashindwa kuzirudisha na hata kukana, ikiwemo
kuwaomba radhi wanachama kwa kitendo cha usaliti," alisema na kuongeza
kuwa anawashangaa baadhi ya wanachama ambao si waaminifu ndani ya chama.
Mbele ya waandishi wa habari, Kiabo aliwataja waasisi hao wa CCJ na
fedha walizochangia kwenye mabano kuwa ni pamoja na Dk. Harrison
Mwakyembe (sh 300,000), Samuel Sitta (sh 500,000), Anne Kilango (sh
400,000), Nape Nnauye (sh 100,000), Paul Makonda (sh 100,000) na James
Lembel (sh 400,000) ambao kwa sasa ni miongoni mwa wanachama wa CCM
wanaotajwa kuwa na makundi ya urais.
Wengine ni Amina Katemi (sh 300,000), Alex Kisumo (sh 300,000),
Baraka Seif (sh 300,000), Sospeter Banigwa (sh 300,000), Saleh Omari (sh
300,000), Sarah Patrick (sh 200,000), Daniel Mwaijojeli (sh 200,000),
Dk. Ngonyani (sh 300,000), Elisha Eliya (sh 200,000), Emanuel Magonja
(sh 200,000) na Asma Watosha (sh 300,000).
Pia wamo, Kulwa Lulelema (sh 50,000), Hamadi Maduku (sh 100,000),
Flavian Nkya (sh 100,000), Gulam kutoka Zanzibar (sh 150,000), Hamad
Ferej (sh 200,000), Ally Harun (sh 50,000), Masudi Kangi (sh 100,000),
Gumbo (sh 150,000), Idd Kiriwe (sh 100,000), Innocent Makala (sh
200,000), Jacob Msambya (sh 200,000), Ishelula (sh 150,000), Kipute (sh
200,000), Joseph Kashindye (sh 200,000) Kamala Ng’ombe (sh 200,000) na
Daniel Malongo (sh 50,000).
Alisema
ni vyema wakati huu kuelekea uchaguzi CCM ianze kujisafisha ili wale
mamluki waumbuke na wasipewe nafasi ya kugombea wakati ukifika
Makonda
alipoulizwa kuhusiana na madai hayo alijibu kuwa anaelewa kuwa mchezo
huo unachezwa na vibaraka kwani suala hilo halina uzito ndani ya chama.
Alidai
kuwa suala la kuondoa watu wanaotumiwa na Lowassa kukihujumu chama
hicho halijibiwi. Alisema ni muhimu kuelewa kuwa wapambe wote wa Lowassa
watatoka na watakapomalizika atashughulikiwa yeye kichama kwani ndiye
tatizo.
“Wapambe
wote watoke na watakapoisha tutashughulika na bosi wao anayewatuma...
ninajua hawajajipanga ndiyo maana wamekurupuka na kuja na hoja rahisi,"
alisema.
Alisema
wanamtaka Lowassa akanushe kuwatumia hao watu. Kwa Nape, alisema
yalishajadiliwa na mjadala kufungwa ndani ya chama, hivyo madai hayo si
mapya hawezi kuyazungumzia.