Mwalimu Msaidizi wa Shule ya Msingi Kivule ya Manispaa ya Ilala, Wilson
Muhemba akionyesha ubao ulioandikwa gharama za uchangiaji wa mtoto
anayeingia darasa la kwanza jana.
Picha na Pamela Chologola.
======
Msimu wa uandikishaji watoto wanaoanza darasa la kwanza,
umeanza, huku kukiwa na malalamiko lukuki hasa kutokana na michango
inayotozwa kwa watoto wanaokwenda kuanza darasa la kwanza.
Itakumbukwa, Novemba 7, 2012, Naibu Waziri katika
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
anayeshughulikia Elimu, Majaliwa Kassim Majaliwa alisema bungeni mjini
Dodoma kuwa ni kosa kwa walimu wakuu kutoza fedha kwa watoto wanaoanza
darasa la kwanza na atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua kali za
kisheria.
Majaliwa alikuwa akibu swali la nyongeza la Mbunge
wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, alisema kama ni michango ni ile
iliyokubaliwa na wazazi wenyewe, Kamati za Shule lakini pia na kupata
baraka za mamlaka husika za elimu katika Halmashauri au Wilaya.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Serikali, inaonekana
kupigwa kumbo huku wazazi wakishangaa michango hiyo, ambayo mingine
haieleweki na mingine ilikubalika kupitia kamati za shule.
Tozo la kujiandikisha:
Wazazi wa watoto waliokwenda kujiandikisha katika
Shule ya Msingi Kivule wameulalamikia uongozi wa shule hiyo kuwachagisha
kiasi cha Sh40,000 kwa ajili ya watoto wanaojiunga darasa la kwanza
jambo lililosababisha watoto kushindwa kujiunga.
Malalamiko kama hayo ambayo yako kwenye shule
mbalimbali, pia yaliibuka katika Shule ya Msingi Mtoni, Dar es Salaam
kwa wazazi kulalamikia kutozwa Sh33,500 wakati mjini Morogoro katika
Shule ya Msingi Kambarage iliyopo Kata ya Chamwino katika Manispaa ya
Morogoro michango ilifikia Sh50,000 kwa kila mzazi.
Katika Shule ya Msingi Kivule, Dar es Salaam,
wazazi wameulalamikia uongozi kukataa kuwaandikisha watoto na wazazi
kulazimishwa kutoa Sh40,000 ndipo watoto wao waandikishwe kuanza darasa
la kwanza mwaka huu.
Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Mwalimu Mkuu
Msaidizi wa shule hiyo, Wilson Muhemba, alikana madai hayo na kusema
anachoelewa yeye ni mchango wa Sh15,000 kwa ajili ya kujenga madarasa ya
shule mpya ambayo ilipitishwa kwenye kikao cha wazazi.
Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha; Rozi Mwing’a
alisema alifika shuleni hapo kwa ajili ya kuwaandikisha watoto wake
wawili aliambiwa atoe mchango wa Sh40,000 kwa kila mtoto hivyo
imesababishia kushindwa kuwaandikisha watoto hao.
Alisema wanachangia michango wa ujenzi wa shule
Sh15,000, mchango wa fulana Sh6,000, mchango wa mafunzo ya awali
Sh6,000, nembo Sh1,000 na ulinzi ni Sh5,000.
Mwing’a alisema mchango mwingine wa fomu Sh5,000,
kupima uzito Sh1,000, picha za pasipoti Sh3000 na mchango wa madaftari
saba Sh1,500.
“Tumeshangazwa kuona tunachangishwa Sh15,000 kwa ajili ya ujenzi
wa madarasa wakati madarasa yameshajengwa, mimi naona huu ni mradi wa
walimu na kamati na bodi ya shule,” alisema Mwing’a.
Mzazi mwingine, Silvester Chacha alisema hiyo
michango wanayochangishwa hawakuwahi kukaa kikao chochote kwa watoto
watakaojiunga darasa la kwanza.
Alisema mwanaye amerudishwa nyumbani hadi hapo
atakapopata kiasi cha Sh 25,000 ili kufikia kiwango cha kiasi
walichopanga walimu hao.
Walimu wajitetea kwa michango:
Mwalimu Mkuu Msaidizi Muhemba alisema yeye
anachojua ni mchango wa ujenzi wa shule mpya na vyoo ambayo ni Sh15,000
iliyopitishwa kwenye kikao cha wazazi walichokaa mwishoni mwa mwaka
jana.
“Hiyo michango mingine mimi siifahamu wala mchanganuo wake siuelewi hivyo anayeelewa ni mwalimu mkuu wa shule.
“Inaonekana hawa wazazi wameunganisha na michango
ya kununulia fulana na hela ya mafunzo ya awali ambayo tulikubaliana na
wazazi ni hiari Sh6,000, mchango wa nembo ya shati, madaftari na hela ya
picha ambazo hizo ni lazima watoe wazazi hawakutakiwa kuchanganya na
Sh15,000 ya jengo ambayo ilikubaliwa na wazazi wenyewe.”
Alisema na suala la watoto kurudishwa haijawahi
kutokea katika shule hiyo. Kama mzazi hana fedha ya kumwandikisha
anaruhusiwa kumwandikisha lakini baadaye analipa fedha hizo kwa
utaratibu utakaowekwa.
Kwa upande mwingine, wazazi waliofika kuandikisha
watoto kwa ajili ya kuanza daraza la kwanza katika Shule ya Msingi Mtoni
wamelalamikia kutozwa Sh33,500 lakini Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Omar
Kitwana amekataa kutoa ufafanuzi kuhusu mchanganuo wa fedha hizo.
Mmoja wa wazazi hao, Subira Ali alisema wameambiwa
ada ya kuandikisha mtoto kuanza darasa la kwanza ni Sh33,500.
Tumeambiwa fedha hizi ni kwa ajili ya madawati, lebo, fulana na mlinzi,
kwa umaskini huu tunashindwa kuandikisha watoto ili kusoma elimu ya
msingi,” alisema Subira aliyeondoka na mtoto, June Hassan bila ya
kumwandikisha.
Mwalimu Kitwana mbali na kukataa kutoa ufafanuzi
wa zoezi la uandikishaji, pia alikataa wanafunzi walioanza darasa la
kwanza wasipigwe picha.
Katika Shule ya Msingi ya Bokoramu ya Temeke, wazazi wanaandikisha watoto kwa Sh35,000 ili kuanza darasa la kwanza.
“Nimetoka kulipia ada hiyo ya usajili, lakini inasikitisha
kwamba licha ya fedha nyingi ambazo wazazi wamekuwa wakitoa lakini
watoto wamekuwa wakisoma wakiwa wamekaa sakafuni,” alisema.
Alitaka Serikali kuweka viwango vya ada ya
uandikishaji vinavyofanana tofauti na ilivyo sasa kila shule kutoza
kiwango chake kwa kisingizio cha Kamati za Shule na Wazazi.
Wakati wazazi wakilalamikia hayo, baadhi ya Wakuu
wa Shule za Msingi, wametoa ufafanuzi wa madai yanayotolewa na wazazi
kuhusu malipo ya michango ya shule kwa watoto wao wakati wa
kujiandikisha wakisema agizo hilo ni la Serikali.
Akizungumza jana na mwandishi wa gazeti hili,
mmoja kati ya wakuu hao ambaye aliomba kutotajwa jina na shule
anayofundisha kwa madai ya usalama wa ajira yake, alisema mwaka jana
Wizara ya Elimu ilitoa agizo hilo kwa Halmashauri zote nchini.
“Kwa hapa Dar es Salaam, kila shule iliitisha
vikao na wazazi, mimi kwa hapa shuleni kwangu tuliainisha mahitaji
kadhaa yanayotakiwa kuchangiwa na mzazi na jumla ya mahitaji yote
ilifikia gharama ya sh 16,000 kwa mahitaji ya sare ya shule (fulana),
kulipia mitihani, mchango wa dawati na uji,” alisema na kuongeza:
“Baada ya hapo tukawashirikisha wazazi kwenye
vikao vyetu mbalimbali na kukubaliana ila wanaolalamika ama ni wageni au
hawakufika kwenye mikutano ya kuweka utaratibu wa maendeleo ya shule na
hawaelewi kama kuna makubaliano ambayo hufanyika kwenye vikao vya
wazazi.”
Aidha, aliongeza kuwa gharama hizo hazichukuliwi
kama malipo ya ada kwa mwanafunzi anayesajiliwa kujiunga na darasa la
kwanza. “Kwa hivyo ni suala la uelewa tu kwa wazazi na wala hakuna
utapeli unaofanyika,” alisema mkuu huyo.
Serikali Dar yatoa ufafanuzi:
Akitoa ufafanuzi mbele ya wazazi hao, Ofisa
Taaluma Mkoa wa Dar es Salaam, Kiduma Mageni alisema hakuna shule yoyote
inayoruhusiwa kutoza pesa kama malipo ya kusajili mwanafunzi anayeingia
darasa la kwanza.
Mageni alisema pamoja na kuwepo kwa makubaliano ya
michango hiyo, bado haiwezi kuwa kikwazo kwa mwanafunzi asipate haki ya
kuandikishwa kuanza shule.
“Ni marufuku na hairuhusiwi michango hiyo. Kwanza
ni lazima mtoto aandikishwe kisha iangaliwe namna ya mzazi kumudu
gharama hizo kwani uwezo wa wazazi unatofautiani
M wingine hata Sh10,000 tu hana kuilipa kwa mwaka
halafu umpe michango ya Sh30,000 au zaidi atawezaje,” alisema Mageni kwa
kauli ya kuchukizwa.
Mjini Morogoro, wazazi wenye watoto wanaoanza darasa la kwanza
katika Shule ya Msingi Kambarage iliyopo Kata ya Chamwino katika
Manispaa ya Morogoro jana walipigana ngumi na bakora kutokana na
kubishania ulipwaji wa mchango wa Sh50,000 kwa kila mzazi.
Vurumai hiyo ilitokea mbele ya Mbunge wa Morogoro
Mjini, Abdullah Aziz Abood aliyekuwa katika ziara ya kutembelea shule za
msingi na sekondari katika jimbo lake ili kujionea uandikishaji wa
watoto unavyofanyika.
Wazazi wa watoto ambao walikuwa hawajalipa mchango huo, walikuwa wamejikusanya shuleni hapo.
Mmoja wa wazazi, Hamad Hassan alikiri wazazi kukubaliana michango hiyo kutokana na kikao cha Novemba mwaka jana.
Imeandikwa na Raymond Kaminyonge, Pamela Chilongola, Dar, Lilian Lucas, Moro na Mussa Mwangoka, Mbeya, Via gazeti la mwananchi
