WAKUU WA TAASISI ZA USALAMA NCHINI WAZUIWA KUSTAAFU NA RAIS KIKWETE

RAIS Jakaya Kikwete amewaongezea muda wa miaka miwili, wakuu wote wa Idara za Ulinzi na Usalama nchini, RAI Jumatano lina habari kamili. 
 
Taarifa za uhakika zimeeleza kuwa wakuu walioongezewa muda ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema, Mkuu wa Majeshi Jenerali, Davis Mwamunyange, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman na Naibu Mkurugenzi wa Idara hiyo, Jack Zoka.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili, zilibainisha kuwa idadi kubwa ya wakuu hao walikuwa wamalize utumishi wao kwa mujibu wa sheria mwishoni mwa mwezi huu. Mmoja wa wakuu wa idara hizo nyeti aliyekuwa astaafu mwishoni mwa 
mwezi huu ni IGP Mwema, ambaye awali alishamaliza muda wake, lakini aliombwa kuendelea kushikilia nafasi hiyo kwa miezi sita zaidi.

Imeelezwa kuwa IGP Mwema alikataa kuongezewa muda wa zaidi, lakini aliombwa kukubali na kuwa tayari kuongezewa miezi sita, ambayo ilikuwa inafikia kilele Desemba 30, mwaka huu.

Hata hivyo imeelezwa kuwa hatua ya Serikali kumuacha IGP Mwema na maofisa wengine wastaafu, ingeleta mkanganyiko kwenye uongozi wa Rais Kikwete ambaye amebakiza miaka miwili ya uongozi wake.

Aidha imeelezwa kuwa endapo Rais Kikwete angewateua wakuu wapya wa Idara hizo, ni wazi hao wapya wasingedumu kwenye nafasi zao, kwani kiongozi mpya atakayepatikana kwenye uchaguzi mkuu ni lazima atakuwa na mapendekezo yake na watu wake.

“Lisingekuwa jambo la busara kwa Rais kuteua wakuu wengine wa Idara za Ulinzi na Usalama, wakati amebakiza miaka miwili ya uongozi wake. Hatua hiyo ingeleta mkanganyiko kwenye Serikali yake na hata hao ambao wangepewa majukumu wangejikuta hawakai kwa muda mrefu kwenye nafasi zao, Rais ajaye ni lazima atakuwa na watu wake,” kilisema chanzo chetu cha habari.

IGP Mwema ambaye alikuwa Ofisi ya Polisi wa Kimataifa (Interpol) jijini Nairobi, Kenya, aliteuliwa na Rais Kikwete kushika wadhifa huo mwaka 2006 akichukua nafasi ya Omar Mahita ambaye alistaafu.

IGP Mwema anachukuliwa kama mmoja wa viongozi wa juu wa Jeshi hilo aliyelifanyia mapinduzi makubwa.

Mapinduzi hayo ndani ya Jeshi la Polisi, yamekuwa yakisifiwa na wasomi na wanasiasa, ambapo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema IGP Mwema amefanya maboresho makubwa ndani ya Jeshi la Polisi na kwamba anastahili kuendelea kuliongoza jeshi hilo, hadi mwaka 2015.

“Tangu tupate uhuru, Tanzania haijawahi kupata IGP wa aina ya Said Mwema, amefanya maboresho, ulinzi shirikishi pamoja na mambo mengine mengi. Mwema ndiye aliyeweza kubadilisha Jeshi la Polisi na kufanikiwa kupunguza uporaji katika maeneo mbalimbali kama yale ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, wizi katika benki ni yeye aliyesimama kidete kutokomeza hayo, ukweli ni huo kwamba Mwema hana mfano. Siku hizi ukiangalia sifa za RPC utagundua ni wale ambao wamepitia ngazi mbalimbali, yaani amejenga safu imara ya uongozi,” alisema Dk. Bana.

Pamoja na hayo Dk. Bana alipoulizwa kuhusiana na matukio ya uhalifu ambayo hayajapatiwa ufumbuzi, alieleza kuwa hata siku moja mipango haiwezi kuzaa matunda leo na kwamba ni ngumu kumaliza uhalifu, kwa sababu hata mataifa mengine hayajafanikiwa kwa mara moja.

Kwa upande wake, Profesa Ibrahimu Lipumba ambaye pia ni mwanasiasa, alisema Mwema ni IGP wa pekee ambaye wakati wowote yuko tayari kuongea na mtu na kuyasikiliza matatizo ambayo mtu anayo.

“Ni mtu ambaye unampigia simu wakati wowote anapokea na hata ukitaka kuonana naye yuko tayari na anaweza kukusikiliza bila hiyana. Ni mwepesi wa kushauri, si mtu wa kutumia ubabe, Mwema ni mtu wa kutumia busara. IGP Mwema amekumbana na changamoto nyingi, amejaribu kuanzisha ulinzi shirikishi, amekumbana na wakati mgumu sana kwa matukio ya uhalifu mengine ya watu kupoteza maisha katika mikutano mbalimbali, watu kumwagiwa tindikali haya yote na mengine yameleta sura mbaya kwa utendaji wa jeshi la polisi, lakini yeye amejitahidi sana kupambana nayo,”alisema Profes Lipumba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Helen Kijo Bisimba, alisema ni ukweli ulio wazi kwamba IGP Mwema amefanya mabadiliko makubwa ndani ya jeshi la polisi.

Alisema kamanda huyo wa polisi amefanya mambo mengi mazuri, lakini tatizo kubwa yamefichwa na matukio ya uhalifu yaliyojitokeza hivi karibuni.

“Amefanya vizuri lakini amekumbana na wakati mgumu. Tumeshuhudia mambo mengi mazuri mfano kaanzisha ulinzi shirikishi, wakati fulani polisi waliadhibiwa kwa tuhuma za rushwa. Pamoja na hayo akiwa kama binadamu alikumbana na mambo kadhaa yaliyochafua sifa yake kama yale ya watu kutekwa, kuvamiwa, kuumizwa na hata kuuawa na hakuna wahalifu waliochukuliwa hatua na tume zilizoundwa kuchunguza matukio hayo, hali hiyo imesababisha kumuondolea sifa zake njema, lakini pamoja na masuala yote ni IGP bora,” alisema Bisimba
 
Chanzo:Rai Jumatano


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo