MAMLAKA
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kampuni za simu za mikononi,
zimewataka wateja watakaokumbwa na tatizo la kuvujishwa kwa taarifa za
simu, kuripoti kwenye vyombo vya dola ili hatua zichukuliwe.
Aidha
imeelezwa kuwa ingawa kumekuwa na mashine za kuzuia taarifa za siri za
simu za mikononi kutovuja, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za simu
wasio waaminifu wamekuwa wakihujumu wateja kinyume cha sheria kwa
kuchezea teknolojia isivyopaswa.
Hadhari
hiyo imekuja kukiwa na wimbi la matumizi mabaya ya simu za mkononi
nchini, ikiwemo matumizi ya teknolojia kutoa hadharani mawasiliano ya
siri ya watu.
Miongoni
mwa matukio ya hivi karibuni, ni taarifa zilizoanikwa kwenye mitandao
ya kijamii dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto,
zikionesha mawasiliano ya siri anayodaiwa kufanya na watu mbalimbali
yakidaiwa kuwa ni ya kuhujumu chama chake.
Matumizi
mengine ni aliyodai kufanyiwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, ambapo
pamoja na namba za simu kadhaa kudai zinamtumia ujumbe wa matusi, pia
alidai upo ujumbe wa matusi unaotumwa kwa watu na namba inayojitokeza
ikionesha ni ya mbunge huyo suala alilosema juzi limemchafua kisiasa na
kijamii.
Akizungumza
jana na mwandishi juu ya matukio hayo, Meneja Uhusiano wa TCRA,
Innocent Mungy, alisema kampuni za simu zinaongozwa kwa mujibu wa sheria
hivyo hakuna itakayokubali kutoa taarifa za siri za mteja kwa kuwa ni
hatari kwao.
Sheria husika ni ile ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010 inayotoa kinga kwa mteja.
“Ninachojua
ambacho kinaweza kuonekana na kupatikana kutoka katika kampuni hizo
tena kama zikiombwa na Polisi ama vyombo vya usalama kufanya hivyo kwa
kulinda usalama wa taifa, ni kuelezwa siku fulani uliwasiliana na nani
na saa ngapi na kampuni zinaweza kuchapa taarifa hiyo na kuitoa bila
kueleza kilichozungumzwa wazi wazi,” alisema Mungy.
Mungy
alisema kampuni za simu zina utaratibu wa mafundi wake kuingia chumba
cha kuhifadhi taarifa za siri, na ikiwa mtu ana uhakika namba ya kampuni
fulani imetumiwa visivyo, anapaswa kutoa taarifa Polisi ili hatua
zichukuliwe kwa kuwa hilo ni kosa la uhalifu wa mtandaoni.
“Naomba
ieleweke kwamba haiwezekani mtu asikilize maongezi ya mtu na mtu, ama
kusoma ujumbe mfupi wa simu za mkononi, ingekuwa hivyo wafanyabiashara
wakubwa wasingefanya biashara wala taarifa za ulinzi na usalama wa nchi
zisingekuwa siri leo, watu waondoe hofu na ikiwa mtu katendewa hivyo
kweli, aende Polisi kupata haki yake,” alisisitiza Mungy.
Ofisa
Mawasiliano wa Kampuni ya simu ya Zantel, Monica Ekelege akizungumzia
suala hilo, alisema mafundi katika kampuni za simu wana uwezo wa kuona
mawasiliano ya mtu na mtu ikiwa wanatafuta kitu na kujua namba ya mtu,
lakini hawawezi kutoa mawasiliano hayo kwa kuwa kampuni nyingi zina
mashine ya kuzuia siri.
“Huu
ni uhalifu kama uhalifu mwingine, mtu anaweza akachokonoa chokonoa na
kuibuka na njia nyingine ya kuvujisha taarifa za mtu, huyu akibainika,
sheria haimwachi lakini kwanza kwa kuwa sisi tunafanyakazi chini ya
sheria inayomlinda mteja na siri zake, ana mamlaka ya kutushitaki lakini
lazima awe na uthibitisho na kuanzia Polisi,” alisema Ekelege.
Ekelege
alisema uhalifu mwingi wa simu wanaoufanya watu, wanatumia udhaifu wa
baadhi ya mawakala waliozembea kutumia vielelezo stahiki katika kusajili
namba za simu, na sasa baadhi wanatumia mwanya huo kufanya uhalifu.
Kuhusu
watu wanaotumia simu kutuma ujumbe wa matusi au kufanya uhalifu
mwingine kama vile utapeli, Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando,
alisema mara nyingi wanaofanya vitendo hivyo ni wenye simu ambazo
hazijasajiliwa kwa kufuata utaratibu unaopaswa.
Alisisitiza
waathirika wa vitendo hivyo kutoa taarifa Polisi na kampuni yao itatoa
ushirikiano kubaini wahusika ili hatua zichukuliwe.
-Habari leo
-Habari leo