Afisa elimu sekondari wilaya ya Makete Jacob Meena
===
Kutokana na matokeo ya kidato cha nne mwaka jana nchi nzima kuwa mabaya, wanafunzi wa kidato cha nne wilayani Makete wametakiwa kujiandaa vyema na mitihani ya taifa iliyopo mbele yao ili wafaulu vizuri
kauli hiyo imetolewa na Afisa elimu sekondari wilaya ya Makete mkoa wa Njombe, Jacob Meena ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 10 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Iwawa
Katika hatua nyingine Bw Meena ameagiza kuanzia Januari mwakani wanafunzi wote wa kike waanze kulala shuleni hata kama hakuna vitanda, inawezekana kutandika magodoro chini na wanafunzi wakalala chini wakati utaratibu wa kutafuta vitanda unafanywa
Amesema hivi karibuni walitembelea Ikuwo sekondari na kukuta wanafunzi wote wa kike wakilala kwenye mabweni ambayo hayana vitanda na wametandika magodoro chini na wanalala, hivyo haoni sababu ya kuzuia hilo kwa kuwa niawezekana wakalala chini wakati suala la vitanda linashughulikiwa
Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuinua kiwango cha elimu hapa wilayani pamoja na wanafunzi hao kupata muda mzuri zaidi ya kujisomea kwa kuwa watakuwepo katika mazingira ya shule
Meena amewasisitiza wanafunzi hao muda huu mchache uliobaki wajisomee kwa bidii kuhakikisha wanafaulu ipasavyo kwani mitihani tayari imefika wilayani na inawasubiri wao
"Mitihani yenu tayari imefika na inawasubiri ninnyi, tunategemea mmejiandaa vizuri, soma kwa bidii kwa muda huu mchache uliobaki ili ufaulu" alisema Meena
Akishukuru hotuba ya mgeni rasmi mwenyekiti wa bodi ya shule bw. Jasel Mwamwala amewasihi wanafunzi hao kuzingatia yote waliyofundishwa shuleni pamoja na aliyoyasema mgeni rasmi na kuhakikisha akili zao wanazielekeza kwenye mtihani ili wafaulu