RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri
Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said
Mwema kufuatia kifo cha aliyepata kuwa Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha
Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Mstaafu, James Kombe aliyefariki dunia tarehe 22 Oktoba, 2013 katika
Hospitali ya Ocean Road iliyoko Jijini Dar es Salaam akipatiwa matibabu.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyepata kuwa Kamanda
wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani hapa nchini, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mstaafu, James Kombe aliyefikwa na
umauti akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road Jijini Dar es
Salaam” amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
“Nilimfahamu Marehemu James Kombe, enzi za uhai wake, kama Askari
Shupavu, Mtiifu na Mwaminifu aliyejituma vilivyo katika utekelezaji wa
majukumu yake. Kwa hakika sifa hizi ndizo zilizochangia kwa kiasi
kikubwa kupandishwa Cheo na kushika nyadhifa mbalimbali za juu hadi kuwa
Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD); Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC); Mkuu wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), na hatimaye Mkuu wa Kikosi cha Usalama
Barabarani, cheo alichokitumikia hadi alipostaafu mwaka 2010”,
ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais Kikwete amesema utumishi huu uliotukuka wa Kamanda James Kombe
ndani ya Jeshi la Polisi, ni wa kujivunia na wa kupigiwa mfano ambao
Askari Polisi wengine hawana budi kuuiga ili Jeshi letu la Polisi
liendelee kuaminiwa, kuheshimiwa na kupewa ushirikiano stahiki kutoka
kwa Wananchi.
“Kutokana na Msiba huu, ninakutumia Salamu za Rambirambi wewe Mkuu wa
Jeshi la Polisi, Said Mwema kwa kumpoteza Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Polisi Mstaafu, Marehemu James Kombe. Natambua fika kuwa licha ya
kustaafu kwake, ushauri wake kwa Jeshi letu la Polisi ulikuwa bado
unahitajika sana”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
Aidha Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema
kumfikishia Salamu zake za Rambirambi kwa Familia ya Marehemu James
Kombe. Ameihakikishia Familia hiyo kuwa yuko pamoja nao katika
kuomboleza kifo cha Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia yao.
Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema
aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu James Kombe.
Ameiomba Familia ya Marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati
huu inapopitia machungu ya kuomboleza Msiba wa Mpendwa wao.