Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwafurahia wasanii chipukizi Gosbert
Bwere(4) anayepiga ngoma na mwenzake Nyambari Mganga(5) walipokuwa
wanamtumbuiza muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa
Nansio,Ukerewe, kwa ziara ya kikazi.
======= =======
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa siyo kazi ya Serikali kuviokoa
vyama vya ushirika kutoka kwenye madeni kwa sababu shughuli za ushirika ni za
sekta binafsi na mali
ya wanachama wenyewe.
Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa makosa ya ushirika na wezi wa baadhi
ya viongozi wa vyama vya ushirika hatimaye yanabebeshwa vyama vya siasa.
Kama namna ya
kuwasaidia wananchi, Rais Kikwete amewataka viongozi mbali mbali wa mikoa
kuwasaidia wananchi ili kupata viongozi waadilifu na waaminifu na wala siyo
wezi kama ilivyo sasa kwa vyama vingi vya ushirika.
Rais Kikwete
ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo, Jumamosi, Septemba 7, 2013, wakati
alipopokea Ripoti ya Maendeleo ya Mkoa wa Mwanza kwenye Ikulu Ndogo mjini
Mwanza kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo.
Rais Kikwete
aliwaambia viongozi hao wa Mkoa wa Mwanza: “Tumewahi huko nyuma kulipa madeni
yote ya vyama vya ushirika. Nia ilikuwa kuvisaidia vyama hivyo na wanachama
wake kujipanga upya na kupata uhalali wa kuweza kukopa fedha za kjuendesha
shughuli zao. Lakini sasa, vyama hivyo, vimerudi kule kule kwenye madeni.”
Alitoa mfano wa
Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Pwani kama moja ya vyama vya ushirika ambavyo
madeni yake yalilipwa na Serikali lakini sasa kina deni kubwa zaidi kuliko hata
lile lililolipwa na Serikali.
“Wale watu wa
Pwani walikwenda kukopa na benki moja ikakubali kuwapa fedha. Wameshindwa
kulipa na ule ushirika nadhani utakufa. Njia bora kwa vyama vya namna hiyo ni
kuviachia vife tu kwa sababu havina faida yoyote kwa mkulima.”
Aliongeza:
“Vyama vya ushirika siyo mali
ya Serikali. Ni mali ya wanaushirika
na hivyo ushirika ni sekta binafsi. Lakini hakuna shaka kuwa baadhi ya viongozi
wa vyama vya ushirika wanatesa wananchi. Wanakopa fedha kwenye mabenki lakini
wanashindwa kuzirudisha fedha hizo na hilo linapotokea Serikali inalaumiwa kwa
hali hiyo.”
Rais alikuwa anatoa maelekezo yake baada ya kuambiwa kuwa Chama cha
Ushirika cha Nyanza cha Mkoa wa Mwanza kilikuwa kinakamilisha mpango wa kukopa
kiasi cha sh bilioni saba kutoka Benki ya Raslimali Tanzania (TIB) kwa ajili ya
kununulia pamba.
Lakini aliwaambia viongozi hao: “Uamuzi wa kukopa ama kutokukopa ni wa
kwenu. Nyanza ni mali yenu, wezi waliopata kukibebesha madeni chama hicho
mliwachagua nyie wenyewe. Fedha ni zenu lakini hatimaye athari za makosa yenu
yanaiathiri Serikali na hata vyama vya siasa.”
“Kuna wakati viongozi wa Chama cha Nyanza walipata kuuza godown ya thamani
y ash milioni 600 kwa sh milioni 50 tu. Hawa ni wezi wa mchana wanaoiba kweupe.
Wanaiba lakini wanataka Serikali iwasaidie. Kwa nini? Nadhani kazi yetu kama
viongozi ni kuwasaidia wananchi kupata viongozi adilifu na aminifu siyo wezi,”
alisema Mheshimiwa Rais Kikwete na kuongeza:
“Tatizo ni kwamba hata sisi viongozi tunakataa kuwashughulikia wezi kwa
sababu hawa ni watu maarufu na wakati mwingine baadhi ya viongozi wanakula nao
na jambo hilo limekuwa tatizo kubwa sana. Tunavifikisha vyama vya ushirika
mahali ambako sina uhakika kama bado ni mali ya wakulima. Wakulima wanakutana
na ushirika wakati wa kuchagua viongozi tu na baada ya hapo wakulima
hawaonekani tena.”