Mwanasheria
Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud Othman (Pichani) ameshangazwa na
mwanasheria mwenzake Tundu Lisu kwa kutofahamu madhumuni na malengo ya
mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yaliozaa serikali ya umoja wa kitaifa.
Kauli ya Mwanasheria huyo aliitoa katika baraza la wawakilishi wakati
akifafanua baadhi ya mambo ya kisheria baada ya wajumbe wa baraza hilo
kumtaka afanye hivyo kufuatia kauli ya ya Tundu Lisu aliyoitoa bungeni
wiki hii.
“Sasa
kuja kwa haya yametuonesha kwamba kuna wenzetu kumbe wana fikra kwamba
Zanzibar iliwahi kutawaliwa.
Maana mtu anaposema marekebisho ya 10 ya
Zanzibar yamjitangazia uhuru maana yake ana fikra na huyu ni
mwanasheria mtu kafika mpaka kuwa mbunge anayeaminika na chama chake
lakini anasema kwa kufanya hivyo Zanzibar imejitangazia kuwa huru kwani
tuliwahi kutawaliwa?,” alihoji Othman.
Akijadili
bajeti ya wizara ya makamu wa rais wa jamhuri ya muungano, huko Dodoma
Mbunge wa Singida Mashariki wa Chama Cha (CHADEMA) Tundu Lisu
alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa Zanzibar imefanya katiba
kwa kujitangazia kuwa ni nchi.
Othman
alisema marekebisho ya katika ya Zanzibar yalikuja baada ya hoja
nyingi ambazo hazikuwa na majibu katika muungano ambayo ilikuwa ikisema
ni Zanzibar ni sehemu ya muungano, lakini kama nini mkoa? Shehia?
Kata? au kijiji?, haya hayakuwa na jibu katika katiba ya muungano.
Kufuatia
maridhiano Zanzibar ndipo wazanzibari wakamaua kufanya kukufikia
marekebisho ya 10 ya katiba yao ambayo ilifafanua kuwa zanzibar ni nchi
na ndivyo ilivyo kwa sababu haikuwahi kutawaliwa kama ambavyo baadhi ya
wanasiasa wanavyofikiria.
“Marekebisho
ya 10 ilichofanya ni kusema kwamba ikiwa mtu hatambui, maana ilikuwa
imeshaonesha dalili kwamba kuna wengine hawatambui hilo tena wakubwa.
Sasa marekebisho ya 10 yalipokuja ni kufafanua tu, kama kuna mtu
hatambui sisi wenyewe tunajitambua” alisema mwanasheria huyo huku
akiungwa mkono na wajumbe kwa kupigiwa makofi.
Huku
akishangiriwa na wajumbe wa baraza hilo mwanasheria mkuu alisema
hakuna mtu ambaye atawazuwia kusema “Aaah katiba yenu isiwe namna gani
au isiwe hivi na ndio maana unakuta katiba za muungano zipo nyingi
lakini kila mmoja ina muundo wake kwa mujibu mlivyokubaliana nyinyi
wenyewe.”
Mwanasheria
mkuu alisifu muungano wa miaka mingi wa Uswizi ambao unatambulika na
kuigwa duniani kutokana na kufuata misingi imara iliyowekwa na wananchi
wenyewe.
Alisema
muungano ambao umedumu na unasifiwa ni Swiss Federation kwa sababu
umeanza tokea mwaka 1292 na umekwenda kwa mafahamiano hadi mwaka 1874
wakatunga katiba ambayo wameifanyia mapitio upya mwaka 1999 na nchi hiyo
ina serikali 26, lugha nne rasmi na ndio muungano amabo umedumu na
nchi ambayo ni imetulia duniani.
Mwanasheria
huyo alisema mashirika yoye ya kimataifa yapo Uswizi kwa sababu ya
muungano huo uliotumilia na kwa sababu umekuwa na misingi imara ya
kuhakikisha muungano ule unaweza kuhimili mabadiliko yoyote yatakayokuja
ya kisiasa.
“Mheshimiwa
Naibu Spika nitumie fursa hii hapa hapa niseme wakati tupo katika
mchakato wa maoni ya katiba nadhani ni wakati mzuri kuiweka sawa ile
misingi ya muugano kama Uswizi,”na kuongeza: “Wakati mwengine napata
wasiwasi nasema hii khofu yangu niiseme hapa kwamba tunaanza kubishana
kuhusiana na watunza nyumba wawe wangapi, waendeshaji nyumba wawe
wangapi, wawili, watatu, wanane au watano? Lakini tatizo letu la msingi
mimi nadhani ni nyumba yenyewe iweje. Kama tunaamua kuishi, maana mfumo
wa sasa hivi mmoja anaishi nyumba kubwa na mwengine mabandani huko
uwani huo sio utaratibu tunao.”
Aidha
aliwaambia wajumbe hao kwamba wanzanzibari wana mambo ya msingi ya
kujadili kuliko kuzungumzia idadi ya watunza nyumba akimaanisha kero za
muungano zilizopo na kushindwa kuafikiwa.
“Kwa
hivyo mimi niwaombe sana waheshimiwa wajumbe, niwaombe na wazanzibari
wenzangu na wananchi wote, kwamba huko mbele tusije tukalaumiana kwamba
tumefanya marekebisho ya 10 kimakosa na tumejitangazia uhuru. Sasa
hivi tuondoe fikra hizo lakini tunaweza kujieleza kwa hoja za msingi na
mambo ya msingi katika hoja hii hapo ndipo tutakapojenga utawala bora
ndani ya muungano,” aliongeza Mwanasheria huyo.
Akitoa
ufafanuzi zaidi kwa wajumbe hao kuhusu muungano Othman alisema hata
suala la uraia limepewa kipaumbele katika katiba ya Uswizi ambapo mtu
anapozaliwa ndipo anapopewa uraia wake.
“Pale
unapozaliwa ndio panapokupa uraia, na kuna mengi ambayo nadhani tatizo
liliopo kwa wenzetu ni kwamba hawajifunzi kwamba muungano ni kitu
gani. Muungano ni suala ambalo nchi mbili mnapoungana, nchi zilizokuwa
huru ni suala la makubaliano na mtakachokubaliana ndicho ambachi
kitakuja katika katiba yenu,” alisema Othman.
Othman
ambaye ni mwanasheria aliyewahi kuandika waraka (paper) aliyoipa jina
‘masuala ya yasiokuwa na majibu ndani ya muungano’ aliwaambia
wawakilishi hao kwamba maelezo ya Tundu Lisu yamejaa hadaa na yamejaa
upotoshaji tena upotoshaji ambao umepindukia mipaka ya kweli.
“Mimi
nimepata kusoma na kuangalia hiyo hutuba ya Mhe Tundu Lisu… lakini pia
nimeona majibu ambayo yalitolewa na mhehsimiwa Shamsi Vuai Nahodha
aliyesema kuwa maeelzo ya Mbunge Lisu yamejaa hadaa na upotoshaji
naungana naye,” alisisitiza huku makofi ya wajumbe yakitawala ndani ya
baraza hilo.
Tokea
kuanza kwa kikao cha baraza la wawakilishi kwa kiasi kikubwa mijadala
wa bajeti umetawaliwa na suala la muungano ambapo wajumbe wengi
wamekuwa wakiungana na wananchi kudai maslahi zaidi kwa zanzibar
ikiwemo kurejesha kwa hadhi ya rais wa zanzibar na mamlaka kamili ndani
na nje ya nchi.
Imeandaliwa na Salma Said, Zanzibar