MBUNGE wa Viti Maalum, Mariam Msabaha
(CHADEMA) ameitaka serikali kutoa mikopo ya magari kwa mawakili wa
serikali ili waweze kufanya kazi zao kwa wepesi zaidi.
Msabaha alitoa kauli hiyo bungeni
mjini hapa wakati akiuliza swali la nyongeza akitaka kujua ni mawakili
wangapi wa serikali wana nyumba nzuri za kuishi.
Pia alitaka kujua ni lini serikali itaboresha mazingira ya kazi kwa mawakili hao ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria, Angela Kairuki, alisema serikali kupitia Bunge,
imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa watumishi
wake wakiwemo mawakili wanafanya kazi katika mazingira bora na yenye
usalama.
“Katika kutimiza azma hii, serikali
imekuwa ikijitahidi kila inapowezekana kuboresha mazingira ya kazi kwa
mawakili wa serikali kwa kuwapatia vitendea kazi,” alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), alitaka kujua ni kwa nini vitabu vya
rejea ambavyo ni vya masuala ya kisheria haviuzwi kwa mawakili wakiwemo
wa kujitegemea.
Akijibu swali hilo, Kairuki alisema kuwa vitabu hivyo vimekuwa vikichapishwa isipokuwa upatikanaji wake ndio umekuwa mgumu.
Hata hivyo alisema serikali inafanya
mchakato wa kuhakikisha vitabu hivyo vinapatikana kwa urahisi na kuuzwa
kwa wanasheria wote nchini.
