
MAZISHI
ya rasta mmoja maarufu kwa jina la Rasta Gido aliyekuwa dereva wa
bodaboda yameonekana kushika nafasi ya juu katika rekodi ya marehemu
wote waliozikwa Ifakara, Morogoro miaka ya karibuni.
Rasta Gido alipata ajali mbaya ya kugongwa na gari aina ya Fuso, Julai 28, mwaka huu eneo la Ifakara Kibaoni.
Akizungumza
na waandishi wetu juzi, jijini Dar baada ya kurejea kutoka kwenye msiba
huo, mjomba wa marehemu aitwaye Avi Simba alisema msiba huo uliongozwa
kwa imani ya kirasta bila kuhusisha mchungaji wala shehe huku
waombolezaji wakivalia kofia za kirasta zenye rangi za kijani,
nyekundu, njano na nyeusi hali iliyozidisha kuyafanya mazishi hayo kuwa
ya aina yake.
Mbali
na kofia hizo, jeneza la marehemu lilipakwa rangi hizo za kirasta
zilizotajwa hapo juu, hivyo kulifanya eneo lote la msiba kutawaliwa na
taratibu za kirasta.
“Mimi
na ndugu zangu wote tulikaa chini na kukubaliana kuwa marehemu azikwe
kwa imani ya kirasta bila kufuata taratibu za dini yoyote ile,” alisema
mjomba huyo wa marehemu.
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya wananchi waliohudhuria msiba huo
walijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na utaratibu wa mazishi
uliowekwa na ndugu na jamaa wa marehemu ambao ni jamii ya rasta tofauti
na taratibu za dini yake aliyokulia Rasta Gido ya Romani Katoliki.
Hali
iliyoongeza mazishi hayo kuwa ya aina yake ni Wazungu waliofika msibani
hapo sanjari na mwongozaji wa mazishi hayo, Rasta Side ambaye ni
mchumba wa mmoja wa Wazungu hao.
Mbali
na hayo yote, kwenye mazishi, hakukutumika machepe na majembe kufukia
kaburi la marehemu huyo badala yake ilitumika mikono kufanya kazi hiyo
mwanzo hadi mwisho.
Kutokana
na msiba huo, madereva wa bodaboda wa eneo la Kibaoni waliamua
kusitisha shughuli zao ili kuungana na mwenzao katika safari yake ya
mwisho.
Madereva
hao walimlaani vikali dereva wa Fuso aliyemgonga Rasta Gido wakidai
kuwa hakuwa makini barabarani na kusababisha ajali hiyo mbaya.
Nayo
familia ya marehemu ilijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na jukumu
zito la malezi alilowaachia rasta huyo kwani ameacha watoto watatu,
Rose, Neema na Stanislaus ambao wote bado wanahitaji msaada.
Marehemu Rasta Gido alizikwa kwenye makaburi ya familia ya Kibaoni, Ifakara mkoani Morogoro.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Ameni.