Bwana shamba kutoka kampuni ya highland seed growers Iddi Kapteni akitoa mafunzo kwa wakulima wa Makete.
Msambazaji wa mbegu Bw. Tito Tweve akizungumza katika mafunzo hayo
Mkulima naye akichangia katika mafunzo hayo.
======
Wakulima wilayani Makete mkoani Njombe wameshauriwa kuachana na mfumo wa kutumia mbegu za kienyeji katika shughuli za kilimo na badala yake watumie mbegu bora za kisasa zinazozalishwa na kampuni ya Highland seed growers limited ya mkoani Mbeya, kwa kuwa mbegu hizo zimehakikiwa kitaalamu na chuo na kilimo Uyole kuwa zinafaa kwa kilimo mikoa ya nyanda za juu kusini
Hayo yamebainika jana wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima na wagani kutoka vijiji 12 vya wilaya ya Makete yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Francis Chaula
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Kaimu afisa kilimo mifugo na ushirika wilayani hapo Bw. Beda Kusenge amewataka wakulima hao kuzingatia mafunzo hayo pamoja na kwenda kuitoa elimu hiyo kwa wenzao huko vijijini ili waondokane na matumizi ya mbegu za kienyeji ambazo haziwapatii mazao mengi
Amesema katia matumizi ya pembejeo mbegu huchukua asilimia 30 hivyo endapo mkulima atatumia mbegu ambayo si bora ataishia kulalamika na kupata mazao kidogo kila alimapo
Kwa upande wake bwana shamba wa kampuni ya Highland seed growers Bw. Iddi Kapteni akitoa elimu kwa wakulima walioshiriki katika mafunzo hayo amesema huu sio muda wa wakulima kuteseka na kuona kilimo hakifai, na badala yake wanatakiwa kutumia mbegu za kampuni hiyo kwa kuwa zimethibitishwa kitaalam kutumia katika mikoa yote ya nyanda za juu kusini
Amesema ili mkulima apate mazao mengi ni lazima atumie mbegu hizo pamoja na kuwashirikisha wataalamu wa kilimo katika hatua zote, na endapo watafanya hivyo wataona mabadiliko makubwa katika kilimo chao
Ameongeza kuwa kupitia mbegu hizo ni lazima kipato cha mkulima kiongezeke mara dufu huku akiwataka wananchi kuwa makini na mbegu feki endapo zitatokea kwa kuwa hazitawaopatia mazao mazuri na wataishia kuilalamikia kampuni
"Unajua kizuri ndicho kinachoigwa na tunaimani mbegu zetu ni nzuri na endapo wataziiga mnatakiwa kuangalia hii mbegu halisi tunayowapa leo, na ndani yake kuna kakaratasi kenye maelekezo yaote, katunzeni sana katawasaidia pamoja na alama nyingine tutakazowaonesha" alisema Kapteni
Naye msambazaji wa mbegu hizo wilaya ya Makete Bw. Tito Tweve amesema kutokana na mwitikio wa wakazi wa Makete kukubali kubadilika na kutumia mbegu hizo zenye ubora, wanaimani watasambaza ipasavyo kwa wakulima wote wilayani humo kwa bei nafuu hivyo wakulima wakae makao wa kula
Katika mafunzo hayo wakulima hao wameuliza maswali na kujibiwa papo hapo pamoja na kupew mbegu bora za mahindi mfuko wa kilogramu 2 bure kwa ajili ya majaribio