Kamanda wa
Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Kamishina Suleiman Kova,akiongea
na waandishi wa habari kuhusiana na Watanzania kuacha utamaduni wa
kubeba pesa nyingi badala yake watumie mfumo wa kielektroniki wa M-PESA
kwani ni sehemu ya maisha ya mtanzania kwa sasa,wengine kutoka kushoto
ni wafanyakazi wa Vodacom Tanzania.
======== ======= =========
Kamanda
wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Kamishina Suleiman Kova,
amewataka wananchi wenye mazoea ya kubeba fedha nyingi kutoka sehemu
moja kwenda nyingine kuacha tabia hiyo kutokana na sababu za kiusalama.
Kamishina
Kova ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
katika ofisi kuu za polisi kanda maalum ya Dar es Salaam huku
akitanabaisha kuongezeka kwa matukio ya watu kuporwa fedha wakiwa
wanaelekea au wanatoka katika mabenki na wakati mwingine kutokea kwa
vifo.
"Jeshi la polisi linafanya jitihada kubwa kukabiliana na uhalifu wa aina
mbalimbali, tunataka wananchi watupe ushirikiano ili tuweze kupunguza
matukio ya uhalifu, Kazi kubwa ya polisi ni kuzuia uhalifu na sio
kupambana na uhalifu hivyo wananchi wanatakiwa wawe wa kwanza kuzuia
uharifu usitokee". Alisema Kova na kuongeza.
"Kwa wadau mbali mbali katika kuhakikisha usalama wa raia wa nchi leo
tunayofuraha kushirikiana na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom kupitia
huduma ya M pesa katika kuleta suluhisho la uvamizi kwa watu wenye
mazoea yakubeba fedha nyingi kutoka sehemu moja kwenda nyingine,"
Alisema kuwa kuna watu wanadhani kuwa na fedha nyingi ndani au kubeba
fedha nyingi ni ufahari, "Kuna watu wanatabia za kushangaza sana, mtu
anafurahi kubeba pesa nyingi akijiona ni ufahari na hata wakati
mwingine kuwaita watu na kuwaonyesha pesa zao ili wawaogope au kuwasifia
utamaduni huo umepitwa na wakati."
Kova alisema jamii ya sasa inatakiwa kutoka katika mfumo wa matumizi ya
fedha taslim, (Cash Sosiety) na kuwa jamii yenye matumizi ya fedha kwa
njia za Ki elektroniki (Cashless Society) Ili kuokoa trasilimali za
jeshi la polisi na vifo visivyo vya lazima kwa askari au raia.
"Katika
usindikizwaji na polisi kunaweza kukatokea uvamizi ambao unaweza kuleta
mapambano na hatimaye kusababisha vifo, "Nawasihi wote mtumie mfumo huu
maalum wa M pesa katika kuhifadhi pesa zenu na katika kuwalipia
wafanyakazi mishahara yao na hata magawio mengine kwasababu ndio njia
yenye usalama zaidi kuliko kutoa fedha benki na kutembea nazo.
Kwa
kufanya hivyo mtakuwa mmelisaidia jeshi la polisi katika operesheni zake
kwasababu ni mfumo wa kiusalama zaidi hivyo kupelekea uhalifu kupungua
na kutupunguzia sisi gharama za operesheni zetu katika kuhakikisha
usalama wa wananchi." Kwa upande wake Mkuu wa Ukuzaji wa Biashara
M-Pesa, Jackson Kiswaga alifafanua zaidi mfumo huo unaotumia M-Pesa
kufanya kazi.
"Mfumo
huu mpya wa kielektroniki wa kulipa mishahara na magawio kwa njia ya
M-Pesa ni rahisi na ya haraka zaidi. Kitakachofanyika hela zitatumwa
kutoka akaunti yako ya benki kwenda kwenye akaunti inayoitwa Fast
Account ambayo ni ya M- Pesa alafu kwenda kwenye akaunti ya kawaida ya
M-Pesa na hapo ndipo unaweza kulipa wafanyakazi wako kwa kuandika tu
majina yao nambari zao za simu na kiasi kisha kubonyeza kitufe cha
kutumia," alisema Kiswaga.
Alimalizia
kwa kusema kuwa kwa mfumo huu unaweza kulipa wafanyakazi zaidi ya mia
mbili kwa wakati moja na vilviele kwa wafanyabiashara wanaoingiza zaidi
ya billioni moja wanaweza wakajiunga na M-Pesa daraja la tatu (level
three) na kujiwekea fedha zao kwenye akaunti ya M-Pesa na ataweza
kulipa shilingi milioni kumi na mbili kwa wakati mmoja na milioni 50 kwa
siku.