WABUNGE WA VITI MAALUM WAMPINGA SITTA

Wabunge wa Viti maalum wakiwemo Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mheshimiwa Esther Bulaya na Mheshimiwa Zarina Madabida (CCM) wamejitokeza kumpinga Waziri wa Jumuiya ya Africa Mashariki, Mheshimiwa Samwel Sitta kufuatia kauli aliyoitoa kuunga mkono mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba Mpya kuwa Viti Maalum vifutwe Bungeni.

Akizungumza kwenye mkutano wa Chama cha Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG) wa kujadili mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Bulaya alisema “Mara nyingi hawa wabunge waliochaguliwa na wananchi wanalalamikiwa kwamba hawapatikani, lakini sisi wa viti maalumu muda mwingi tuko na wananchi kuangalia changamoto zinazowakabili na kuziwasilisha sehemu husika ili zitatuliwe,”

Aidha, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zarina Madabida alisema “Wabunge wa Viti Maalum wana michango mizuri, pia wana uwezo wa kuzunguka nchi nzima kutatua kero zinazowakabili wananchi.”

Akizungumza katika mkutano huo Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Makinda, alisema “Miaka 50 baada ya uhuru, wanawake hatuna tena sababu na msamaha wa kutokushiriki kwenye zoezi hili muhimu kikamilifu... wanawake tumepata uzoefu wa kutosha, tunayo elimu ya kutosha na tunayo sauti. Kubwa zaidi ya yote tunajiamini.”

“Sisi wachache tuliokusanyika hapa tumebahatika. Ni mithili ya taa za mbele za gari ambazo ndizo humwongoza dereva wakati wa giza. Hivyo, tuna wajibu wa kuyasema matatizo na changamoto zinazowakabili wanawake na makundi mengine kama vile watoto na walemavu hususan wakati huu tunapoandika Katiba Mpya.”

“Bado kuna masuala ambayo sisi kama taasisi tungependa yaingizwe kwenye Rasimu ya Katiba. Ni vizuri tunapoandika Katiba Mpya, mihimili hii hususan Mahakama na Bunge iwiane ili kuleta heshima na kuaminiana zaidi.”


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo