Kata ya Iwawa ilipo shule hiyo.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Iwawa wilayani Makete mkoani
Njombe wamekiri uwepo wa wanafunzi wenzao ambao wanajihusisha na vitendo vya
ngono na wengine wanaishi na virusi vya UKIMWI, licha ya jamii kudhani kuwa
wanafunzi hawawezi kuwa na virusi hivyo kwa minajili kwamba bado ni wadogo
Hayo yamebainika baada ya mtandao huu kufanya mahojiano ya
kina na baadhi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hivi karibuni kwa ruhusa ya mkuu
wa shule hiyo Bw. Christopher Haule hapo kufuatia wananchi wengi wilayani hapo
kudhani kuwa wanafunzi hao hawana maambukizi ya vvu kwa kuwa ni wadogo na
huwenda hawajaanza kujihusisha na vitendo vya ngono
Mwanafunzi mmoja (jina linahifadhiwa kwa sababu za
kimaadili) amesema ana marafiki zake zaidi ya watano ambao wanaishi na virusi
vya UKIMWI na hajui walivipataje, hivyo anaamini wapo wanafunzi wengi ambao
wana maambukizi
Amesema jamii inapaswa kuondokana na dhana potofu kuwa
mabinti ama vijana wadogo hawana vvu waache mara moja kwa kuwa virusi vinampata
mtu yeyote bila kujali umri
“Mtu anayedhani kuwa wanafunzi huwa hawana vvu ni uongo, na
pia waanatakiwa kuacha kujihusisha kimapenzi na wanafunzi kwa madai kuwa hawana
vvu, lakini wakumbuke sheria za nchi haziruhusu kujihusisha kimapenzi na
wanafunzi, jamani Ukimwi upo kwa kila mtu” alisema mwanafunzi huyo
Mwanafunzi mwingine amesema yeye hafahamu kama wanafunzi hao
wenye vvu wanajihusisha kimapenzi na watu kwa kuwa wapo ambao wanaishi na
wazazi wao na wengine wamepanga kwenye nyumba maarufu kama mageto ambao kwa
kiasi kikubwa wako huru kufanya mambo yao kwa kuwa hawana muangalizi
“Ni kweli kabisa wapo wanafunzi wenye vvu wanaoishi wenyewe
kwenye mageto, lakini mimi sijui kama wana wapenzi ama lah, maana ni ngumu
kujua na mimi sipo hapa kwa ajili ya kufuatilia maisha ya mtu, na hao ninao
kwambia kwa kuwa ni marafiki zangu na waliwahi kuniambia kuwa wanaishi na vvu”
alisema mwanafunzi huyo(jina tunalo)
Mmoja wa mwanafunzi aliyezungumza na mtandao huu
Mwanafunzi upande wa kushoto wa picha hii amemweleza mwandishi wetu kuwa mpenzi wake anamlazimisha kufanya mapenzi bila kondomu
“Mimi kwa upande wangu Kusema kweli nina mpenzi na nilishawahi kupima vvu
mwaka jana (2012) na kujikuta sina maambukizi namshukuru Mungu kwa hilo, na pia
nimekuwa nikifanya mapenzi kwa kutumia kondomu lakini kuna wakati mwingine
hatutumii mimi na mpenzi wangu na mara nyingi yeye ndiyo ananishawishi
tusitumie, na huyo mpenzi wangu si mwanafunzi ni jamaa tu wa pale mtaani kwetu,
na mimi huwa nakwenda home kwake(Nyambani kwake) na wakati mwingine anakuja
geto kwangu, ili atumie kondom huwa namwambia leo ni siku zangu za hatari, hapo ndipo atavaa kondomu” alisema mwanafunzi huyo wa kike ambaye anaishi kwenye nyumba ya
kupanga
Akizungumzia suala hilo, diwani wa kata ya Iwawa Benjamin
Mahenge alikiri kuwepo kwa tatizo la ukimwi kwa kila mtu, na kuongeza kuwa hata
wanafunzi wapo wenye vvu ingawa ni kwa kiasi kidogo ukilinganisha na miaka
iliyopita na pia wapo wanafunzi wanaojihusisha na vitendo vya ngono, na ambao wameshabainika wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria
Diwani wa kata ya Iwawa Benjamin (kushoto) akizungumza na mwandishi wa habari
"Unajua ni ngumu mwanafunzi kuniambia mimi ama kiongozi mwingine kuwa anajihusisha kimapenzi na mtu lakini kwako mwandishi kasema, mimi ninaomba wawe wawazi ili tuweze kuwasaidia hasa pale linapojitokeza tatizo hasa mimba kwa kuwa hawawataji wahusika" alisema Mahenge
Mahenge amesema huu ni muda wa jamii kubadilika na
kuondokana na dhana potofu kuwa wanafunzi hawawezi kuwa na vvu, na pia wawaache
wanafunzi hao wasome na si kuwarubuni na kujikuta wakifanya nao mapenzi
Pia amesema wapo wanafunzi katika kata yake ambao wamepanga
na uangalizi wao si mzuri kwa kuwa wanajiamulia mambo yao wenyewe hata kama si
mazuri kutokana na kukosa uangalizi wa watu wazima
Moja ya nyumba iliyoko Makete mjini amayo wanafunzi wamepanga
“Unakuta mwanafunzi kajipangia kwenye chumba chake, yeye
ndio kila kitu, akitaka kusoma haya, akitaka kwenda disco hakuna wa kumuuliza,
hii ni hatari pia” alisema Mahenge