MTOTO MDOGO WA KIKE AUAWA KINYAMA MKOANI MBEYA

 
MTOTO mmoja wa kike ameuawa kinyama kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kisha kunyofolewa macho na ubongo wake.
Tukio hilo la kikatili, limetokea mwishoni mwa wiki eneo la Idiwili kata ya Isuto wilaya ya Mbeya vijijini mkoani hapa.
Mtoto huyo wa kike, asiye na hatia, mwenye umri wa miaka miwili, aliyejulikana kwa jina la Lilian Nex Kasonso, alikatishwa uhai wake kwa makusudi kisha mwili wake kutelekezwa chini ya mti.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo waliozungumza mwandishi wa habari hii wamesema kuwa, Mama wa mtoto huyo, alimwacha mwanae akiwa salama mikononi mwa bibi yake kisha yeye kwenda kutafuta kuni.
Punde, Bibi yake Lilian, naye alienda kuchota maji mtoni huku akimwacha mjukuu wake akiwa na furaha tele, ndipo majitu hayo makatili, kwa makusudi walimteka mtoto huyo kisha kutokomea naye pasipo mtu kuwaona ama kuwashitukia.
Mama wa marehemu aliporejea na kuuliza mwanae yupo wapi, ndipo ikawa kama amewazindua ndugu waliokuwepo jirani kisha ikapigwa nkolo ya kutaka msaada, wananchi wakasambaa na kuanza kumsaka mtoto Lilian. 
Wakiwa katika harakati za mahangaiko ya kumtafuta, wananchi wanasema, walimuona mtu mmoja kwa mbali akiwa amevalia shati jeupe ndani ya mashamba ya kahawa, na walipojaribu kumfuatilia aliwatoroka na walipofika eneo ambalo alionekana mtu huyo, lahaula, wakaona majani ya kahawa yakiwa juu ya mwili wa mtoto Lilian.
Wakaanza kuona miguu, na walipofunua zaidi, wakashtuka kumkuta Lilian akiwa amefariki, huku mwili wake ukiwa hauna tena macho na ubongo ukiwa umechokonolewa na kwa dhihaka kubwa ya wauaji hao, wakaweka gogo la mti lenye ukubwa wa mkono wa mtu mzima juu ya kichwa chake.
Askari polisi walitaarifiwa na kufika eneo la tukio ambapo baadhi yao wakiwa wamevalia sare la Jeshi hilo, wakajikuta wanaangua kilio na kusema kuwa hawajawahi kuona mauaji ya kikatili namna hii.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Diwani Athumani, amesema halitasalia jiwe juu ya jiwe kwa waalifu wa aina yeyote wanaofanya matukio mkoani hapa. 

chanzo:jambotz blog


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo