MWANZA, Tanzania.
KATIBU wa
NEC, Itikadi na Uenezi, CCM, Nape Nnauye amesema japokuwa mabadiliko ni
muhimu kwa maisha ya binadamu lakini lazima kila yanapohitajika yafanywe
kwa umakini mkubwa ili yasiwe na madhara.
Amesema ni
kutokana na sababu hiyo, ndiyo maana CCM imekuwa ikisisitiza umakini na
busara kubwa vitumike wakati huu ambao Tanzania ipo katika mchakato wa
kupata katiba mpya.
Nape amesema
miongoni mwa mambo ambayo CCM inaona kwamba lazima yatazamwe kwa
umakini na busara kubwa kabla ya hatua ya mwisho, ni kuhusu Tanzania
kuwa na serikali ngapi, ambapo rasimu ya kwanza ya Katiba inapendekeza
serikali tatu.
Nape ambaye
alikuwa akizungumza wakati akifungua Kongamano la Vijana mkoani Mwanza
lililofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu (BOT) Kapripoint
jijini Mwanza, juzi, alisema, kwa upande wake CCM kuhusu kipengele hicho
cha Tanzania kuwa na serikali ngapi, msimamo wake ni serikali mbili.
"Sisi CCM
tunapotangaza msimamo wetu kwamba nchi hii inastahili kuwa ya serikali
mbili, haina maana kwamba tunadharau au kuwaona wapuuzi wanaopendekeza
ziwe tatu, la, msimamo wetu huu tunaueleza kwa hoja ili hatimaye jamii
ya Watanzania ikiziona zina mantiki watuunge mkono", alisema Nape.
Aidha Nape
alisema, umuhimu wa kuwa makini na kutumia busara katika jamii kuhitaji
mabadiliko unatokana na kwamba jamii ikiyapokea kwa pupa huambulia
yasichotarajia, ikiwemo machafuko au uongozi wasiohitaji kwa ajili ya
kukidhi matakwa yao ya maendeleo.
Nape alisema
katika pupa ya kutafuta mabadiliko, zipo baadhi ya nchi kama Misri
ambazo hadi sasa zimekosa utulivu kutokana na kupokea vibaya dhana ya
mabadiliko, wakaingia mitaani lakini bila kuchukua tahadhari, hatimaye
wamejikuta mabadiliko waliyopata nayo hawayataki tena, wanataka mengine.
Akifafanua
alisema, CCM inatambua kwamba, muundo wa serikali mbili ndio utafaa
katika kudumisha Muungano, kuliko serikali tatu ambazo CCM inaona kwamba
mbali ya kuwa mzigo zaidi kwa wananchi, pia ni kuongeza changamoto juu
za zile zilizopo sasa kwenye muungano.