UKISHAKUA mtu mzima jiepushe na kusema uongo, maana utakuaibisha. Hebu
jiangalie wewe na utu uzima wako, unawekwa kati, unasutwa, unajaziwa
watu, mtaa unasimamisha shughuli zote na kuja kukushuhudia wewe. Aibu
sana!
Ronald na Juliana ni wanandoa kwa mwaka tano sasa. Katika kipindi hicho, wamefanikiwa kuwa na watoto watatu. Kila mmoja ni mchapakazi, maana hakuna anayemtegea mwenzake katika kuchangia pato la familia.
Mume (Ronald) ni ofisa mikopo wa benki moja jijini Dar es Salaam na mkewe anaendesha kampuni yake binafsi ambayo inahusika na utoaji wa huduma za usafi wa nyumbani. Mwanamke huyo ni shujaa, kwani alianza kama mchezo lakini ushupavu wake umemuwezesha kupata wateja kila kona.
Kwa sasa, kampuni hiyo, ina tenda ya kusafisha nyumba za vigogo wengi, ofisi nyingi, kadhalika ina hoteli na gesti nyingi ambazo kila siku iendayo kwa Mungu huzisafisha. Kinachomsaidia Juliana ni umakini wake katika kazi, kwani huwa habweteki ofisini kusubiri ripoti na fedha zinazolipwa na wateja wake.
Amekuwa na kawaida ya kuwashtukiza wafanyakazi wake kila eneo la kazi, kuona jinsi wanavyofanya kazi kikamilifu. Hufanya hivyo ili kutopoteza wateja, maana mteja asiporidhika na namna nyumba au ofisi yake inavyosafishwa, atasitisha mkataba mara moja.
Kutokana na uaminifu huo, amejijengea heshima kubwa kwa wateja wake. Wanampenda na kumwamini ndiyo maana hajawahi kupoteza mteja hata mara moja. Uimara huo umemuwezesha kuwa na wateja wengi na amewasaidia vijana wengi kwa kuwapa ajira.
Aprili mwaka huu, ikiwa ni muda mfupi baada ya Sikukuu ya Pasaka, Ronald alimuaga mkewe anakwenda safari Mbeya. Alisema anakwenda Mbeya kikazi na ataendesha gari lake binafsi. Mke hakuwa na ubishi, akamtakia mumewe kila la heri.
Siku ya kwanza ikapita, iliyofuata asubuhi, kama kawaida yake, Juliana alikwenda ofisini kwake, akaweka mambo sawa kisha akaanza ziara ya kukagua wafanyakazi wake. Diary yake ikamwonesha anatakiwa kuanzia Neo Mobo Guest House ambayo ipo Mbezi Mwisho.
Alipofika hapo gesti, alipitia maeneo tofauti ya nje kuangalia jinsi yalivyosafishwa. Baada ya hapo, aliingia ndani, akachukua muda kidogo kwenye korido akiwaelekeza wafanyakazi wake wawili jinsi ya kutumia dawa ya kusafisha marumaru (tiles).
Akiwa katika utoaji wa maelekezo, mlango wa moja ya vyumba vya gesti hiyo ukafunguliwa, akainua macho kuelekea kule sauti ya mlango iliposikika, hakuamini macho yake alipomwona mumewe akitokeza akiwa amevaa taulo. Wakakutanisha macho.
“Ronald,” Juliana alipaza sauti ambayo ilimshtua mume wake. Kuona hivyo naye akarudi chumbani mbio na kujifungia. Hakufungua mlango licha ya mkewe kugonga kwa nguvu. Mke naye akajua akiondoka tu, mumewe atatoroka, ikabidi agande palepale.
Wakati akisubiri, Juliana alimpigia simu kaka yake, akamweleza alivyomfumania mumewe. Kaka mtu bila kulaza damu, akakusanya mabaunsa kisha wakavamia eneo la tukio. Ronald aliendelea kugoma kufungua mlango. Usiku uliingia, watu wakakesha mpaka asubuhi ikawasili.
Asubuhi, kaka yake Juliana alikwenda kutoa taarifa polisi kisha wakafika pale gesti, hivyo kwa amri ya polisi ndipo Ronald alifungua mlango. Juliana alishikwa na hasira kali baada ya kugundua kwamba aliyekuwa na mumewe pale gesti ni rafiki yake kipenzi Maua.
“Maua, yaani pamoja na kukusaidia bado umenisaliti? Kweli rafiki wa kweli ni mama na baba,” Juliana alijikuta akitoa maneno hayo, kwani ni yeye ndiye aliyemkutanisha mumewe na Maua, pale shosti wake huyo alipotaka mkopo wa biashara. Kumbe Ronaldo alikubali kumsaidia kumpa mkopo wa fedha, hakuishia hapo, wakakopeshana na miili yao kabisa.
CHANZO:GPL