Mkuu
wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Vicent Kone akitoa taarifa kwa waandishi
wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya ujio wa Mwenge wa uhuru mkoani
Singida kesho Agosti 9 mwaka huu. Uongozi wa mkoa wa Simiyu utakabidhi
Mwenge huo wa uhuru kwa uongozi wa mkoa wa Singida kwenye kijiji cha
Nyahaa tarafa ya Kirumi wilaya ya Mkalama.Kushoto ni katibu tawala mkoa
wa Singida, Liana Hassan.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu Via MO BLOG.
Mwenge
wa uhuru unatarajiwa kuzindua, kufungua, kuweka mawe ya msingi na
kutembelea jumla ya miradi 62 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni
25.6, wakati wa mbio zake za mwaka huu zinazotarajiwa kuanza kesho
asubuhi mkoani Singida.
Akitoa
taarifa ya ujio wa mwenge huo mkoani Singida, Mkuu wa mkoa Dkt. Parseko
Vicent Kone amesema mwenge huo wa uhuru unatarajiwa kupokelewa kesho
asubuhi katika kijiji cha Nyahaa kata ya Mpambala tarafa ya Kirumi
wilaya ya Mkalama.
Amesema
kuwa uongozi wa mkoa wa Simiyu wanatarajia kukabidhi mwenge huo wa
uhuru kwa uongozi wa mkoa wa Singida kwenye kijiji hicho cha Nyahaa.
Baada ya kukimbizwa katika wilaya ya Mkalama, siku inayofuata utakimbizwa wilaya ya Iramba.
Agosti
11 wilaya ya Iramba utakabidhi mwenge huo kwa uongozi wa halmashauri ya
manispaa ambao nao kesho yake, watakabidhi kwa uongozi wa halmashauri
ya Singida.
Dkt.
Kone amesema mwenge wa uhuru unatarajiwa kumaliza mbio zake mkoani
Singida Agosti 14 mwaka huu katika wilaya ya Manyoni, ambapo Agosti 15
uongozi wa mkoa wa Singida utakabidhi mwenge huo kwa uongozi wa mkoa wa
Dodoma katika kijiji cha Mpedoo cha mkoa wa Dodoma.
Mkuu
huyo wa mkoa, ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujitokeza
kwa wingi katika maeneo yote ambayo mwenge wa uhuru utapitia.
Dkt
Kone amesema “Mwenge wa uhuru uwe ni chachu ya maendeleo yetu, miradi
yote itakayozinduliwa au kufunguliwa, tushirikiane kuitunza ili idumu na
kutuletea maendeleo tarajiwa.
Miradi
yote ambayo itawekwa mawe ya msingi tushirikiane pia katika
kuikamilisha ndani ya muda mfupi na vyema iwe kabla ya mbio za mwenge wa
uhuru wa mwakani”.