MAMA AMUUA MWANAYE KWA KUMCHARANGA NA MAPANGA KYELA


Na Ibrahim Yassin,Kyela.
MKAZI wa kitongoji cha Ndombosya kata ya Itope Wilayani Kyela Mkoani Mbeya Neema Kassika (37) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilayani hapa kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kiume wa kumzaa aliyejulikana kwa jina la Emmanuel mwenye siku kumi na moja kwa kumcharanga na mapanga.

Akizungumza na Blog hii leo Afisa mtendaji wa Kata ya Itope Limi Thomas alisema kuwa alipewa taarifa za mauaji hayo na Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Itope juu ya tukio hilo la aina yake lilitokea siku ya tarehe 19/08/2013 ambapo alifika katika eneo la tukio na kujionea unyama huo.

Alisema baada ya kupewa taarifa ya uwepo wa viashiria vya mauaji aliamua kuita watu kadhaa na kuingia ndani ili kujionea ualisia wa mauaji hayo na kwamba baada ya kuona kuwa mauaji ya mtoto aliyeuawa kwa kucharangwa na mapanga ndipo alipotoa taarifa kwenye kituo kikuu cha polisi wilaya ambao walifika katika eneo la tukio.

Alidai kuwa baada ya polisi kufika katika eneo la tukio wakiwa na daktari waliuchukua mwili huo na kuufanyia uchunguzi  na kuwa mara baada ya uchunguzi waliruhusu familia ya marehemu kuendelea na mazishi huku mtuhumiwa akiwekwa lumande na atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Aliongeza kuwa mara baada ya polisi kuondoka walifika maafisa wa kituo chamsaada wa kisheria kwa wanawake na watoto ambao walitaka kujua tatizo hilo ambapo ofisi yake iliwapa ushirikiano wa kutosha na kwamba watafanya uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo.

Mkurugenzi wa kituo cha msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto wilayani hapa Kyela Pallalegal Unity(KYEPU) Annamaria Mirambo alisema kuwa ofisi yake imeyapokea kwa masikitiko mauaji hayo na kuwa watafanya uchunguzi ili kubaini tatizo lililopelekea mama huyo kuamua kumuua mtoto wake aliyemzaa mwenyewe na kuhakikisha kuwa anapelekwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake.

Baadhi ya wana Kijiji kwa upande wao mbali na kusikitishwa na uwepo wa tukio hilo pia walidai kuwa mwanamke huyo anasadikika kuwa  anatatizo la ugonjwa wa akili na kuwa huenda alitenda kosa hilo bila kujijua kutokana na tatizo alilonalo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo