MAHAKAMA YA SINGIDA YATUPILIA MBALI KESI YA VIONGOZI WA CHADEMA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mjini Singida leo imetupilia mbali kesi iliyokuwa inanawakabali viongozi wawili wa CHADEMA Ndugu Mwita Waitara ambaye ni afisa sera na utafiti makao makuu na mshauri wa chama hicho Dk Kitila Mkumbo. 
 
Katika hukumu yake aliyeisoma mbele ya wakili wa washtakiwa hao Tundu Lissu Hakimu wa Mahakama hiyo Masham alisema kuwa washatakiwa hawana kesi ya kujibu kwa kuwa mashahidi wa serikali walishindwa kuthibitisha aina ya matusi yaliyodaiwa kutolewa na washtakiwa. 
 
Aidha, hakimu huyo alisema kwamba upande wa serikali walishindwa kumleta shahidi muhimu katika kesi hiyo Mwigulu Nchemba aliyedaiwa kutukanwa ili athibitishe kwamba yeye ndiye aliyetukanwa na namna ambavyo matusi hayo yamemuathiri. 
 
Kushindwa kwa Mwigulu Nchemba kufika mahakamani ni kuonyesha kwamba ama hajui kwamba alitukanwa au hakuona kosa lolote alilotendewa na mahakama haiwezi kutoa uamuzi kwa mambo ya kuhisiwa, alisema hakimu huyo. 

Washtakiwa walidaiwa kutenda kosa hilo tarehe 14 Julai mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ndago wilayani Iramba ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo kilikuwa na mkutano wa hadhara. 
 
Kesi hiyo imekuwa ikisuasua mara nyingi kwa upande wa serikali kushindwa kuleta mashahidi mahakamani na kusababisha kesi hiyo kuahirishwa mara kwa mara, jambo ambalo lilikuwa likimkera hakimu wa kesi hiyo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo