Kibao cha shule ya msingi Ndulamo.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya shule ya msingi Ndulamo
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ndulamo Bosco Godigodi akizungumza na mtandao huu ofisini kwake
Mwanafunzi Alexander Marko akizungumzia uwepo wa maji shuleni hapo
Mwanafunzi Timotheo Ibrahim akizungumza na mwandishi wetu
Maji yakitoka kwenye bomba la shule hiyo
========
Kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji katika shule ya msingi
Ndulamo wilaya ya Makete mkoani Njombe hatimaye imetatuliwa baada ya idara ya
maji wilayani hapo kuamua kutilia mkazo suala hilo
Akizungumza na mtandao huu ofisini kwake mwalimu mkuu wa shule
hiyo Bw. Bosco Godigodi Malangalila amesema maji yanapatikana kwa wingi shuleni
hapo baada ya kuyakosa kwa kipindi kirefu hali iliyokuwa inaleta picha mbaya
shuleni hapo
Amesema tatizo hili limeondoka shuleni hapo baada ya idara
ya maji kupeleka mabomba na kuyafunga kufidia yale ya awali yaliyokuwa
yakivujisha maji ilihali yalikuwa mapya hali iliyosababisha kijiji cha Ndulamo
kukosa maji ikiwemo na shule hiyo
Mwalimu Godigodi amesema awali walifanya maandamano hadi
kwenye ofisi za serikali ya kijiji kushinikiza tatizo hilo la maji kuondolewa shuleni hapo na
waliohusika na uzembe uliosababisha maji yasifike shuleni hapo wawajibishwe
“Hivi sasa ndugu mwandishi kuna uafadhali mkubwa kwani maji
yapo, hata waalimu wanaoishi shuleni hapa wanauwezo wa kulima hata kabustani ka
mbogamboga” alisema Mwalimu mkuu huyo
Mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Alexander Marko
amesema kutokana na maji kutoka shuleni hapo yanawasaidia kunywa maji na kunawa
mikono ukizingatia msimu huu ni wa kiangazi
Amesema hivi sasa ile kero ya kwenda kutafuta maji wakati wa
masomo na wakati mwingine wanafunzi kuja na maji ya kunywa shuleni kwa sasa
haipo kwa kuwa yapo maji ya kutosha
Naye mwanafunzi mwingine Timotheo Ibrahim amesema hivi sasa
usafi wa vyoo ni mzuri tofauti na awali lakini pia hata mazingira ya shule
yamekuwa masafi kwa kuwa maji hayo hutumia kupigia deki madarasani na vyooni
Katika hatua nyingine mwalimu Godogodi amesema ujenzi wa
nyumba ya mwalimu uliokuwa ukamilike mwezi huu, hivi sasa unatarajiwa
kukamilika mwezi Septemba mwaka huu kwa kuwa ujenzi huo utaendelea kwa kasi
baada ya maji kufika shuleni hapo
Amesema ujenzi huo ulisuasua kutokana na kukosekana kwa maji
shuleni hapo lakini kwa kuwa kila kitu cha ujenzi hivi sasa kipo ujenzi huo
utakamilika mwezi Septemba