NA DANIEL NYASSY.
MSHUKIWA wa ulanguzi wa mihadarati Jumanne alijisalimisha kwa utawala wa kaunti ya Mombasa baada ya kusakwa kwa mda wa miezi mitatu.
Afisa mkuu
wilayani Jomvu Bw Kennedy Gitonga alisema kwamba Bw Hassan Babu
anayeshutumiwa kwa uuzaji wa kokeni na heroini eneo zima la Jomvu
alijisalimisha mbele ya wazee wa mtaa na naibu wa Chifu wa Miritini Bw
Kombo Matano.
Wananchi walilalamika vikali kwamba Bw Babu alikuwa akilindwa na maafisa fulani wa polisi aliokuwa akiwalipa.
“Ilionekana
kwamba ni kweli mtuhumiwa alilindwa na polisi kwa sababu ilikuwa vigumu
kumkamata na hata tulipomshika, alitoroka kutoka korokoroni kwa njia ya
kiajabuajabu,” alithibitisha Bw Gitonga.
Alisema
ilimbidi kuuandikia barua utawala wa kaunti pamoja na wakuu wa polisi
kuwapa makataa ya siku saba kumtoa Bw Babu “ama sivyo kungewaka moto,"
alisema.
Bw Babu
alijitokeza ndani ya muda huo wa makataa. Alikwenda kwa wazee na naibu
wa chifu na kutia saini kuapa kwamba ataachana na biashara hiyo haramu.
“Aliletwa
kwangu ambako pia alitoa ahadi kama hiyo na kutia saini stakabadhi
Fulani. Sasa tunamtumia na anatusaidia kuwasaka wengine aliokuwa
akifanya biashara nao,” alisema Bw Gitonga
Mbunge wa
eneo hilo la Jomvu Bw twalib Badina muwakilishi wa wodi Bw Karisa Nzai
wamejitolea kumpeleka Bw Babu kwenye kituo cha kurekebisha wahusika wa
dawa za kulevya, aliongeza Bw Gitonga.
Vilevile,
watengenezaji wa pombe haramu ya chang’aa na wauzaji zaidi ya 50
wamejisalimisha kwa mkuu huyo wa tarafa huyo kwa mda wa wiki mbili,
alisema Jumanne.
Misako
“Hii ni
kufuatia elimu nyingi kwa jamii vijijini, kwenye mabaraza na hafla
nyingine. Pia, tumeweka mkazo na misako ya mara kwa mara kwa hivyo,
wafanyabiashara hiyo haramu wameona hawana pa kukimbilia,” alisema Bw
Gitonga.
Miongoni mwa
waliojisalimisha ni 20 kutoka kijiji cha Miritini Station, 20 kutoka
kijiji cha Kwa Matee, 15 kutoka kijiji cha Bahati na wengine kutoka mtaa
duni wa Bangladesh.
“Pia
tumehusisha sana shirika la Nacada na kitengo cha mvinyo kwenye vita
hivi. Tunawataka wahusika waache biashara hii na kujihusisha na biashara
mbadala,” alisema Bw Gitonga.
“Tunawataka
waanzishe biashara haramu. Tumewataka wajiunge kwenye makundi ya 10-20
na watafute mahali pa kufanya biashara halali na tutawasaidia,” alisema
Bw Gitonga.